Kalamu zenu zitumike kuelimisha maradhi mbali mbali kwa jamii.

Afisa mdhamini wizara ya habari, Utalii na mambo ya kale Khatib Juma Mjaja akitoa mada katika mafunzo kwa waandishi wa habari wa PPC juu ya namna ya kuripoti na kujikinga na maradhi ya mripuko ikiwemo COVID-19.

NA HABIBA ZARALI, PEMBA.

 

 

WAANDISHI wa habari Kisiwani Pemba, wameshauriwa kujikita katika kuandika habari sahihi na zilizofanyiwa utafiti hususan zinahusiana na Afya ili kuiwezesha jamii kuelewa maradhi mbali mbali yanayotokea ikiwemo ya mripuko.

Ushauri huo ulitolewa na Ofisa Mdhamini Wizara ya Habari , Utalii na mambo ya kale Pemba , Khatib Juma Mjaja huko katika Ukumbi wa Tasaf Chake Chake Kisiwani humo wakati alipokuwa akifunguwa mafunzo kwa wanachama wa PPC yanayohusiana na maradhi ya mripuko ikiwemo Covid 19.

Alisema kunakuwepo na maradhi mbali mbali ya mripuko ndani ya jamii lakini wananchi wamekuwa hawayaelewi mambukizo wala kujikinga kwake kutokana na Waandishi kutokuwa na utamaduni wa kuandika habari hizo kwa usahihi.

Alifahamisha waandishi wa habari ni watu wanaokubalika na kuaminiwa na jamii iliokubwa hivyo ni lazima wanachokiandika kuhusiana na mambo mbali mbali ikiwemo za Afya ziwe na uhakika kwa kuzifanyia utafiti ili kuepuka upatoshaji na kuwajengea hofu wengine.

“ Nyinyi muliko kwenye tasnia hii muhimu ya habari kumbukeni jamii inawaamini sana hivyo ni muhimu kile munachokieleza kwao kiwe ni cha uhakika ili kuepusha kuwatia hofu watu wanaosoma ama kusikiliza taarifa munazozitowa katika vyombo vyenu ,”alisema Mjaja.

 

 

Alieleza kuwa kipindi kigumu kilichopita cha mripuko wa maradhi ya Corona (Covid 19) jamii iliokubwa ilikuwa inasikiliza taarifa zinazotolewa na watu mbali mbali kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya taarifa zilikuwa sio sahihi na zilikuwa zinawajengea hofu wananchi na kuwaletea taharuki.

Alisema habari  mzuri ni ile inayotoka kwa watu maalumu waliothibitishwa na mamlaka husika kutowa maelezo yanayohusiana na habari fulani hususan zinazohusiana na afya ya jamii na sio kusikia kwa watu wasio wasiohusika na kukurupuka kuandika kwa vile chombo fulani kinahamu kitowe habari hiyo mwanzo jambo hilo ni hatari kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

“ Andikeni habari kwa kufuata maadili ta kazi zenu na musikurupuke tafuteni taarifa kupitia vyombo husika na ikiwezekana fanyeni utafiti japo mdogo ili anaeisoma taarifa ama kuingalia kwenye vyombo vyenu aweze kuifurahia na hilo pia mutavijengea heshima vyombo vyenu na nyinyi wenyewe,”alieleza.

Kwa upande wake mratibu wa maradhi ya mripuko kutoka Wizara ya Afya Pemba, Hamad Hamad Simba, wakati akitowa mada kwa wanachama hao wa Klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC) , alisema waandishi wa habari wanayodhima kubwa ya kuielimisha jamii juu ya maradhi mbali mbali kupitia kalamu zao kwani yapo maradhi mengi ya mripuko ambayo wananchi hawayaelewi .

Alieleza kuna uwezekano wa Wananchi kuambukizwa maradhi ya mripuko kwa kutojuwa chanzo chake wala kujikinga kwake kutokana na kuwa hana taarifa sahihi juu ya ugonjwa huo kwa vile hajapata maelekezo kutoka kwa vyombo vya habari ambao wanauwezo mkubwa wa sauti zao kusikika kuliko Wizara ya Afya.

“ Ninacho wahakikishia sisi Wizara ya Afya tuko tayari kufanyakazi na nyinyi wakati wowote juu ya kuielimisha jamii juu ya maradhi mbali mbali kwani kalamu ina uwezo mkubwa wa kupeleka taarifa kwa haraka kwa jamii popote pale ilipo,”alisema Simba.

Alifahamisha kuwa yako maradhi mbali mbali kama vile homa ya Dengue,Chikungunya, malaria nk, lakini jamii iliokubwa haijawa na ufahamu wa kutosha juu ya mardhi hayo na  taaluma ya kijikinga nayo lakini kupitia vyombo vya habari wakiamuwa ni rahisi kufika taaluma hiyo kwa  jamii.

Simba , alisisitiza waandishi wanapotowa taarifa zinazohusiana na afya wajaribu kutafuta maelezo kutoka kwa watu husika na sio kuandika habari zao kwa kusikia sikia kwani  sio kila mtu ni msemaji wa habari za afya kuna watu maalumu waliopewa uwezo wa kutowa Taarifa za magonjwa fulani.

Alisema muda mdogo aliofanya kazi na vyombo vya habari aliona kuwa wanahabari wanamaadili na kanuni za kazi zao kama walivyo wao ndani ya Wizara ya Afya hivyo aliwasisitiza kuandika habari kwa kufuata misingi hiyo ili kuepusha kuipotosha jamii na kuijengea hofu.

Nao washiriki wa mafunzo hayo waliiomba  Wizara ya Afya kuwa na utamaduni wa kuvitumia vyombo vya habari kutowa taaluma zinazohusiana na maradhi mbali mbali na wasisubiri mpaka kuwe na mripuko wa maradhi ndio wakaanza kuvitumia vyombo hivyo.

Mafunzo hayo juu ya maradhi ya mripuko ikiwemo COVID19 , yaliandaliwa na PPC kwa ufadhili ya Umoja wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC).