Mikutano ya PPC yawaibua wagonjwa 20 wenye TB -2019.

 

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WATU 20 wamegundulika kuugua ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kati ya watu 375 waliochunguza afya zao mara baada ya kumaliza kwa mikutano ya kuelimisha jamii kuhusu TB inayoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kisiwani Pemba, Mratibu wa Klabu hiyo Mgeni Kombo Khamis alisema kuwa, kwa kipindi hicho tayari wameshatoa elimu ya TB kwa watu 6,467.

Alisema kuwa, wakati wanaendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi na kuwahamasisha wapime afya zao, waligundua watu 20 wenye ugonjwa wa TB kisiwani Pemba kati ya 375 waliochunguzwa.

“Klabu ya waandishi wa habari Pemba kwa kushirikiana na Kitengo cha homa ya Ini, Ukoma, Kufua Kikuu na Ukimwi tunaendelea kutoa elimu kwa jamii na tunapomaliza mkutano tu watu wanakuja kupima, wengine wanatufuata ofisini kwa siku nyengine.”, alisema Mratibu.

Alisema kuwa, tayari wameshazifikia shehia 13 kisiwani Pemba, visiwa vinne, madago mawili, masoko matatu, dahalia tano, nyumba ya kurekebisha Tabia (Sober House) moja na Mochuari (sehemu zipopikwa pombe) moja.

 

“Tayari tumeshakwenda kutoa elimu ya TB kwenye visiwa vya Kojani, Makoongwe, Mwambe Shamiani na Kisiwa Panza, hii ni kuhakikisha tunawaibua wenye ugonjwa huu wapate tiba mapema”, alisema.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko kwa shehia na sehemu wanazotoa elimu ya TB, Mratibu huyo alisema kuwa yapo makubwa, kwani kwa sasa watu wamehamasika na kushawishika kwenda kupima afya zao kwa wingi.

“Zamani wakati tunapita kwenye mashehia kutoa elimu ya TB watu walikuwa hawataki kupima, lakini kwa sasa tunashkuru wanakuja na wanatoa ushirikiano mkubwa”, alifafanua.

Mgeni aliishauri jamii kuwa tayari kuchunguza afya zao, ili kupata tiba mapema kwa yule ambae atagundulika, kwani TB ipo na inaambukiza.

“Jamii ni muhimu kuchunguza afya zenu, ili koitokomeza TB, matibabu yapo na dawa zipo zinatolewa bure mahospitalini na kwenye vituo vya Afya”, alisema.

Aidha aliwashauri waandishi wa habari watoe elimu ya TB kwenye vyombo vyao, kwani ni jukumu lao kuielimisha jamii, jambo ambalo litasaidia sana kuwafikia wanajamii wengi kwa muda mfupi.

Wakati PPC ilipowafikia wananchi wa shehia ya Bopwe Wete walisema kuwa, elimu hiyo imewasaidia sana kutoka hatua moja kwenda nyengine na kusema kwamba watawafikishia ujumbe wengine, ili na wao waweze kufaidika.

“Tumefaidika sana kupata elimu hii, angalau atakaejihisi na dalili za TB atachukua kikopo cha kutilia makohozi au atafika hospitali kuchungua kwa njia nyengine”, walisema wananchi hao.

Kwa upande wake sheha wa shehia ya Bopwe Ramia Said Rashid alishukuru kupata elimu hiyo kwenye shehia yake, kwani imewasaidia wananchi kujua athari, dalili za ugonjwa huo na jinsi unavyoweza kuambukiza wengine na kusema kwamba anaamini watapima ili wajue afya zao.

“Kwa kweli nimefarijika sana wananchi wangu kupata elimu hiyo, naamini itasaidia sana, pia nawashukuru wananchi wangu kuitikia wito na kuhudhuria kwa wingi”, alisema sheha huyo.

Mradi wa Kuelimisha Jamii Kuhusu TB unatekelezwa na PPC kwa kushirikiana na kitengo shirikishi cha Homa ya Ini, Ukoma, Kifua Kikuu na Ukimwi chini ya Ufadhili wa Mfuko wa Fedha ya Dunia (Global Fund).