Monday, October 18

Soko la ajira linaendelea kukubalika kwa wahitimu wa Mamlaka ya Amali hivyo vijana wajiunge ili kupata ujuzi.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

AFISA Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salim amesema, Soko la ajira linaendelea kukubalika kwa wahitimu wa Mamlaka ya Amali, hivyo ipo haja ya vijana kujiunga na kupata ujuzi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Afisa huyo alisema, wamekuwa wakitoa vijana wengi na wenye ujuzi kupitia vyuo vya amali ambao wanafanya kazi ndani na nje ya nchi.

Alisema kuwa, ni vyema kwa vijana kujiunga na vyuo vya amali kwa lengo la kujipatia ujuzi kwenye fani mbali mbali, kwani soko la ajira linawakubali wahitimu wenye fani hizo.

“Kwa kweli tuna vijana wengi waliohitimu mafunzo ya elimu amali ambao wamejiajiri na kuajiriwa ndani na nje ya nchi, soko la ajira ndio ushuhuda wetu, tunajivunia sana kwa sababu wanapata kujikomboa kiuchumi”, alisema Mdhamini huyo.

Afisa huyo alisema kuwa, mafanikio hayo yanayopatikana kwa wahitimu hao ni kutokana na kuwepo kwa vifaa vya kufanyia mazoezi, jambo ambalo linawasaidia kupata ujuzi kwa vitendo.

Akizungumzia chuo cha Mamlaka ya Amali Daya Mtambwe Wilaya ya Wete Afisa huyo alieleza, kitaanza kusomesha kozi tano, ambapo watachukua wanafunzi wasiopungua 150 kutokana na walimu waliopo.

“Maombi ni mengi sana, lakini tunaanza kuchukua wanafunzi si chini ya 150 kwa kila awamu kutokana na walimu tulionao kuwa ni haba”, alieleza.

Alifafanua kuwa, chuo hicho kina mabweni, huduma mbali mbali ikiwemo maji safi na salama, nyenzo za kufundishia pamoja na za kufanyia mazoezi, kwa lengo la kutoa wanafunzi wenye ubora ambao watakubalika zaidi katika soko la ajira.

Akizungumzia masharti ya kujiunga na chuo hicho alisema, ni mtu yeyete mwenye elimu kuanzia kidato cha nne na kuendelea na kusema kuwa hawatochukua waliomaliza kidato cha pili, kwani elimu ya lazima kwa Zanzibar ni kidato cha nne.

Aliwaomba wananchi waendelee kuikubali Serikali yao na kuiunga mkono, kwani imekuja na dhana mpya ya uchumi inayofanana na Zanzibar ya sasa.

“Tuna uchumi wa buluu, Wizara yetu tuna dhima kubwa ya kuwaelezea wazanzibari, tuna boti si zaidi ya tano katika eneo la mvumoni kwa ajili ya kufanyia mazoezi”, alisema.

Aidha aliwasisitiza wananchi wawe wazalendo wa nchi yao, kwani vifaa hivyo vimenunuliwa kwa fedha nyingi, hiyo wavihifadhi na kuvilinda vitendea kazi na miundombinu ya chuo kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa, Wizara ina lengo la kuwakomboa vijana, hivyo ushirikiano unahitajika katika kuhakikisha maisha katika jamii yanakuwa mazuri.

Baadhi ya wazazi walisema kuwa, ni faraja kubwa kwao kujengwa chuo hicho, kwani vijana wao watasoma na kupata ujuzi wa fani mbali mbali, jambo ambalo litawasaidia katika maisha yao ya kila siku.

“Hapa ni karibu afadhali sio kama kuitafuta elimu hiyo nje ya kisiwa hiki kama ilivyo kwa vyuo vyengine, tunaamini vitatoka vipaji vizuri na vijana watajikomboa kiuchumi”, walisema.

Kijana mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa mkaazi wa Limbani Wete, chuo hicho kitasaidia sana vijana, kwani wengi wao wanapomaliza kidato cha nne hawana kazi ya kufanya na hatimae kujiingiza kwenye makundi hatarishi.

Chuo hicho kinatarajia kufundisha kozi ya uvuvi, upishi, kilimo cha kisasa, gereji, utengenezaji wa matofali na ICT, ambapo wameshawapa walimu mafunzo, ili waanze kazi ya kuwafundisha vijana hao.