Wednesday, September 22

Haya ni maeneo matano ya kuvutia kutembelea duniani

Dunia imejaliwa maeneo mazuri na ya kuvutia kuyatembelea. Kwa sababu ya ukubwa wa dunia yenyewe sio rahisi kujulikana na kufikika na kila mtu.

Yapo maeneo ambayo ni mazuri na yanafikika kirahisi yanayotumika kama vivutio kwa watalii na yako ambayo ni mtihani kuyafikia.

Kwa yale yanayofikika mengi yanatumika kama vivuti vya Utalii namkusaidia kuingiza mamilioni ya dola kwa nchi ama Mamlaka inayoyasimia.

 

Kwa sababu ya uwingi wa maeneo haya ya kuvutia, sio kazi rahisi kuweza kuyaainisha na kuyaorodhesha, lakini kwa uchache BBC inakuletea orodha ya maeneo matano ambayo ni ya kuvutia duniani na kuyatembelea ni kuweka historia ya kipekee kwa namna yalivyo na yanavyovutia kwa macho.

1: Cappadocia, Uturuki

Eneo hili ni la kipekee sana duniani, linaundwa na mawe yenye muuondo wa kipekee. Watu walioishi hapo miaka hiyo, walitumia mawe hayo kutengeneza makazi chini yake. Baadhi ya muundo wa mawe hayo yanatengeneza mapango madogo yanayoweza kukaliwa na watu wachache wakaishi.

TU

Yapo mawe yenye muundo wa Makanisa, nyumba na hotel na ni eneo linalopendezeshwa kwa kuzungukwa na Maputo juu, Maputo ya rangi tofauti tofauti na kuzidi kuleta mvuto wa macho.

Kwa namna eneo hili la Cappadocia lilivyo unaweza kudhani limehamishwa na mawe yake kutoka sayari nyingine na kuletwa hapo.

Ni eneo la kuhistoria linalopatikana Central Anatolia, katika mjimbo ya Nevşehir, Kayseri, Aksaray, Kırşehir, Malatya, Sivas na Niğde nchini Uturuki na Miezi ya Julai na Agosti, hufurika watalii kutoka kila pembe ya dunia

Mbali na mawe, kuna maeno ya kihistoria mengi na pembeni kumezungukwa na huduma zote muhimu kuanzia uwanja wa ndege, mahotel makubwa na huduma za afya. Kukaa kwa siku tatu hapo inaweza kukugharimu kiasi cha dola 350 mpaka 600

2: Fukwe ya Whitehaven, Australia

Whitehaven beach hii ni fukwe ya kushangaza yenye urefu wa kilometa saba, inayopatikana kwenye kisiwa cha Whitsunday, nchini Australia.

Ili kukifikia kisiwa hicho unatumia boti, ndege za majini ama helkopta kutoka fukwe jirani ya Airlie Beach, bandari ya Shute au kisiwa jirani cha Hamilton.

AUS

Inatajwa kwamba, ndiyo fukwe iliyopigwa picha zaidi duniani, karibu mitandao na tovuti nyingi za picha kwa upande wa picha za fukwe basi zimekusanya picha kutoka fukwe hii.

Fukwe hii ina mchanga mweupe zaidi ambao asilimia 98 ni silica, unaoelezwa kuletwa ufukweni miaka zaidi ya milioni iliyopita.

Upekee wa fukwe hii ni kwamba hata jua liwake namna gani, mchanga wake hauwi wa moto, haushiki joto, hauunguzi na kufanya uweze kutembea peku ama kulala kwenye mchanga bila shaka yoyote na kufurahia madhari ya maji na mawingu ya blue kando ya maji.

Pamoja na uzuri huo na pia mchanga wake kutumika kwa ajili ya kusafisha vito vya thamani kama vya madini, mchanga wake unaweza kuharibu vitu vya umeme kama simu na kamera. Ukiwa hapo ogopa simu yako kuiweka kwenye mchanga, lolote linaweza kutokea.

3: Mabwaya ya Fairy, Scotland

Unaweza kuwa umewahi kuona mabwawa mengi ya kuogelea, yapo ya asili na yapo ya kutengenezwa ambayo utayaona mengi kwenye majumba ya watu ama mahoteli makubwa. Lakini ‘the Fairy Pools’ nchini Scotland ni mabwawa ya kipekee yanayoundwa na mto unaotuamisha maji kwenye eneo lenye mawe na muundo wa ajabu.

JOHN ALLAN/GEOGRAPH

CHANZO CHA PICHA,JOHN ALLAN/GEOGRAPH

Mifereji ya maji yanayotoka kwenye milima ya Cuillin kuingia kwenye mto Brittle kwa kumiminika kwenye mawe na kutengeneza ‘water falls’ na vibwawa ambavyo kwa macho vinavutia kuangalia na kupiga picha.

Wenye uwezo wa kuogelea aji ya baridi na ya mwituni, basi eneo hili linawafaa sana.

Eneo hili la mabwawa ya Fairy lililopo karibu na kijiji cha Carbost lina ukubwa wa kama kilometa 2.4 na inakuchukua dakika mpaka 40 kulitembelea kwa miguu hasa kwenda kwenye eneo lilipo bwawa kubwa na kurudi.

Utachagua mwenyewe kupita njia ngumu sana, ngumu kiasi ama rahisi unapotaka kutalii kwenye eneo hili. Ni sehemu inayotumika sana kwa ajili ya kushangaa na upigaji wa picha.

4: Hifadhi ya Grand Canyon, Marekani

Wakati kwa mfano Tanzania, kwa mwaka watu wanaoingia kutalii kwenye vivutio vyake vyote vya utalii kuanzia mlima Kiliamnaro, hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti, Mikumi nakadhalika hawafiki milioni 2 kwa mwaka, hifadhi hii ya Grand Canyon pekee hutembelewa na watu milioni 5 kwa mwaka.

US

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Hii ni kukuonyesha ni eneo linalovutia sana watu na la kupendeza machoni. Inatajwa kuwa moja ya maeno ya kustaajabisha duniani. Unaweza kujiandaa kushangaa ukifika hapo laikini badala ya kushangaa utastaajabu zaidi. Ni eneo la kipekee klinaloundwa na mawe ya ajabu, kama yametengenezwa kumbe ni ya asili yaliyogunduliwa miaka na miaka.

Upande wa Rim Kusini unatumika sana na watu wanaokwenda kwenye hifadhi hii kwa sababu kuna kila kitu pamoja na miund mbinu muhimu, ingawa wachache wanatumia Kaskazini ambapo uko juu kwa urefu wa futi 1,000, eneo ambalo linavutia zaidi. Wako wanaopanda kwenye mawe hayo kwa kupitia mto Colorado ingawa ni njia ngumu na ya hatari.

5: Kijiji cha Huacachina, Peru.

Huacachina ni kijiji kidogo sana kilichoko kusini magharibi mwa Peru. Kiko katikati ya jangwa kimezungukwa na eneo kubwa la mchanga lakini kimejengwa kwenye eneo dogo lenye mbolea na linaloweza kuotesha mimea.

PERU

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Ni kijiji kinachozunguka kaziwa kadogo na wanakiita Huacachina kwa maana ya rasi iliyojificha, ni kama kilometa 5 kutoka katika mji wa Ica, katika Jimbo la Ica.

Ziwa hili lilikuwa la asili na lilianza kupotea kidogo kidogo katika miaka ya mwishoni mwa 2000s, sasa ili kulilinda, mwaka 2015 wakazi wa eneo hilo walilazimika kujaza maji na ikatangazwa kuwa mwanasayansi Marino Morikawa, kutoka Peru angekuja na mpango kabambe wa kulinda hifadhi na uoto wa asili wa Huacachina.

Kijiji cha Huacachina kina wakazi wa kudumu wanaofikia 100 tu ingawa kila mwaka kinapokea maelfu ya watalii kutoka ndani na nje ya Peru.

Ukiwa Huacachina, utapenda kuona vichuguu vya mchanga unaovutia na michanga hii huvutia michezo mbalimbali, kuna hotel za kifahari na miti migni ya mitende. Kwa waliofika nchi za kiarabu, madhari yake ni kama uko uarabuni.

CHANZO CHA HABARI BBC