Thursday, September 23

MHE. HEMED AZUNGUMZA NA WAFANYABIASHA KUITAFUTIA UFUMBUZI CHANGAMOTO YA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA SALAMA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi inatambua na kuthamini mchango wa wafanyabiashara katika kuunga mkono ujenzi wa miundombinu mbali mbali Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman  Abdulla ametoa kauli hiyo alipokutana na baadhi ya wafanyabiashara waliopo Zanzibar katika  kujadili juu ya  namna bora ya  kuipatia ufumbuzi changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama zanzibar kupitia kikao maalum kilichofanyika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.
Amewapongeza wafanyabiashara hao kwa kutikia wito wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kujitolea katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo ili kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi.
Akizungumzia suala la umuhimu wa maji safi na Salama Makamu wa Pili wa Rais ameeleza kuwa huduma hiyo ni ya muhimu katika maisha ya kila siku ya  binadamu , hivyo ni vyema kukaekwa mazingira mazuri ili iweze kupatikana kwa urahisi huduma hiyo.
Nae waziri wa Maji, Nishat na Madini Mhe. Suleiman Masoud Makame amewashukuru wafanyabiashara hao kwa kuitikia wito huo na kwa kukubali kuunga mkono jitihada hizo ili kuisadia jamii ya wazanzibari kuondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema Mamlaka ya Maji Zanzibar imebadili mfumo wa ukusanyaji wa mapato na kwa sasa wana mfumo mzuri ambao utawasadia kupata fedha za kuendeshea mamlaka hiyo kutokana na makusanyo yatakayokusanywa.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar amesema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyanzo vya maji, upungufu wa pampu ambapo kwa sasa kunahitajika jumla ya pampu 41.
Kwa upande wao wafanyabishara hao wameishukuru Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuthamini mchango wao na kuwapa kipaumbele wafanyabishara katika kuijenga Zanzibar kupitia dhana ya Uchumi wa Buluu.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)