Tuesday, November 30

Dkt. Stergomena Tax: Mfahamu mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Waziri wa Ulinzi Tanzania

Waziri Mteule wa ulinzi, Dkt. Stergomena Tax

CHANZO CHA PICHA,DKT. STERGOMENA TAX/ TWITTER

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri.

Miongoni mwa sura mpya katika baraza hilo la mawaziri, ni mbunge aliyemteua siku chache zilizopita Dokta Stergomena Tax ambaye atakuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa nchini Tanzania.

Dokta Stergomena Tax ni nani?

Dk Stergomena ambaye alizaliwa mwaka 1960, ni mwanamke mwenye heshima kubwa kwenye uga wa kidiplomasia.

Mpaka mwezi uliopita, Dk Stergomena alikuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini ya Afrika (SADC), nafasi aliyoanza kuishikilia tangu mwaka 2013.

Kwa mujibu wa wasifu wa Dk Stergomena, kabla hajaitumikia SADC kwa miaka minane akiwa Mtendaji mkuu, alikuwa mtumishi wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2008 na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Uteuzi wa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki ulikuwa kupanda cheo, kwani kabla ya hapo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.

Stergomena, ambaye ni mama wa watoto wawili, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango mwaka 2006, akitoka kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ubora (BRU), katika Mpango wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Biashara Tanzania (BEST), chini ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji.

Aliwahi pia kufanya kazi katika Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) kama mratibu na mshauri. Kuanzia Mei 1991 mpaka Aprili 2002, alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Fedha, akiwa mhusika mkuu wa usimamizi wa misaada na uratibu (AMC).

Akiwa Wizara ya Fedha, Dk Stergomena alikuwa afisa wa usimamizi wa fedha kabla ya mwaka 1993, alipokuwa ofisa mkuu wa dawati la Benki ya Dunia. Mwaka 1995, alikuwa msimamizi mkuu wa dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Elimu

mm

CHANZO CHA PICHA,AFP

Dk Stergomena ni mhitimu wa shahada ya uzamivu (PhD), aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Tsukuba, Japan akiwa amebobea katika maendeleo ya kimataifa.

Awali Stergomena alisoma shahada ya uzamili ya falsafa ya maendeleo ya kimataifa, Chuo Kikuu cha Tsukuba kuanzia Aprili 1995 mpaka Machi 1997. Shahada ya kwanza aliipata kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia Julai 1987 hadi Machi 1991.

Januari 1984, Dk Stergomena alijiunga na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dodoma, akichukua diploma ya uongozi wa biashara ya kimataifa. Amehusika pia kwenye utengenezaji wa mipango hai ya maendeleo Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Katika wasifu wake, Stergomena anajipambanua kuwa na ubobezi pia kwenye uongozi, usimamizi wa ufadhili na misaada, vilevile diplomasia na majadiliano DC.

Dk Stergomena anaweza kuzungumza lugha tatu kwa umahiri; Kiswahili, Kiingereza na Kijapan. Katika mzunguko wake wa masomo, amepokea mafunzo mbalimbali nchini na nchi tofauti.

Uteuzi wake ni wa kihistoria

Wizara ya Ulinzi haikuwahi kushikwa na mwanamke tangu uhuru kutoka kwa mkoloni.

Hivi karibuni Dkt. Stergomena Tax aliteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania. Uteuzi umekuja baada ya kumaliza muda wake akiwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika – SADC hivyo kuzua tetesi kuwa kungekuwepo mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri.

Malengo yoyote ya kisiasa au kiutawala juu ya teuzi hizi yatafichuka katika utendaji wa walioteuliwa. Namna Rais Samia anavyozichanga karata zake katika baraza la Mawaziri baada ya kifo cha Magufuli, ni wazi kuwa anazichanga kwa kupangua viti ingawa wakaliaji ni walewale.