Tuesday, November 30

WANAFUNZI skuli ya Dodo msingi walia na uchakavu wa madarasa

NA ABDI SULEIMAN.

WANAFUNZI na walimu wa Skuli ya Msingi Dodo Pujini Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, wamewaomba wadau wa maendeleo, viongozi wa jimbo na serikali kuwapatia madawati pamoja na kuwatilia sakafu katika madarasa yao, ili waweze kuondokana na tatizo la uchafuzi was are zao.

Wamesema kukosekana kwa madawati kumepelekea kila siku kufua sare zao, kutokana na kukaa chini pamoja na sakafu kubomoka na kubakia mashimo ndani ya madarasa.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwa nyakati Tafuti juu ya changamoto zinazoikabili skuli hiyo, walisema ubovu wa sakafu ndani ya madarasa yao, inapelekea baadhi ya wanafunzi kupata maradhi ya vifua mara kwa mara kutokana na mavumbi yaliyomo.

Seif Mohamed Kassim mwanafunzi wa darasa la sita skulini hapo, alisema kilio kikubwa cha skuli yao ni ukosefu wa madawa, hali inayopelekea kukaa chini kila siku.

Alisema ni madarasa sita tu yenye madawati huku madarasa 10 yakikosa vikalio, jambo ambalo limepelekea kusoma katika mazingira magumu.

“Wakati mwengine unatamani usifue nguo lakini haiwezekani kutokana na mavumbi yaliyomo ndani ya darasa, hata uwe msafi vipi lazima ukifudi ukafue tu, familia wenyewe masikini kila siku kufua mtihani”alisema.

Naye Naima Hamza Mohamed mwanafunzi wa skuli hiyo, alisema wamekuwa wakisoma kwa shida skulini hapo, kutokana na ubovu wa madarasa hasa sehemu za kukalia kufuatia kuchimbuka mashimo.

“Tokea nyumbani tukipigwa kwa kuchafua nguo mapaka sasa wazazi wanatutizama tu, maana nguo tukirudi hazifai kwa uchafu na lazima tufuwe kila siku”alisema.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa skuli hiyo Juma Othaman Said, alisema ukosefu wa madawati ni shida kubwa kwa skuli hiyo, hali inayopelekea wanafunzi kutokuwa salama wanapokuwepo madarasani.

Alisema kwa sasa skuli yao inamadawati 94 kwa vyumba sita vya kusomoe, huku vyumba 10 vikikosa madawati hayo wakati skuli inawanafunzi 1048.

“Darasa lina mashimo na michanga, mwanafunzi anatoka kwao msafi akifika hapa tayari ameshachafuka, madawati yaliyopo ni kidogo skuli nzima inamadawati 94 kwenye wanafunzi 1048”alisema mwalimu Mkuu.

Aidha alisema kwa sasa skuli ipo katika mazingira hatarishi sana kwa mwanafunzi, huku wakihofia kupata ajali yaa kuvunjika mguu, jambo linalowafanya walimu kuwa katika wakati mgumu.

Hata hivyo alisema kwa sasa skuli hiyo inahitaji madawati 200 ya wanafunzi kwa vyumba 10 pamoja na viti vya walimu, huku wakiwaomba wadau kuitupia jicho la huruma kuwasaidia, ikiwemo kupatiwa bati nyengine kutokana kipindi cha mvua kuvuja.

Afisa Elimu Wilaya ya Mkoani Salum Mkuza Sheikhan, alisema Wizara ya elimu tayari imeshaiweka skuli hiyo katika skuli ambazo zinahitaji matengenezo ya haraka, licha ya wilaya ya Mkoani kua na skuli 36 za msingi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, aliahidi kusaidia mifuko 10 ya saruji kwa ajili ya uwekaji sakafu nyengine ndani ya skuli hiyo.

Alisema kwa kiasi kikubwa skuli ipo katika mazingira hatarishi kwa wanafunzi, huku akiwaomba wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kusaidia madawati pamoja na utiaji sakafu ndani ya madarasa hayo.

Email:abdisuleiman33@gmail.com

MWISHO