Tuesday, November 30

WANAFUZNI zaidi ya 7000 wakimbia skuli na kujiingiza katika ajira za utotoni

 

NA ABDI SULEIMAN.

 

IMEELEZWA uparaji wa Samaki na ubanjaji wa kokoto kwa watoto wa wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, umepelekea wanafunzi zaidi ya 7000 kukatisha masomo katika skuli mbali mbali na kuingia katika ajira hizo.

Hali hiyo imebainika hivi karibuni katika maeneo bandari za wavuvi Tumbe, msuka na shumba, wimbi kubwa la watoto amboa umri wao unawalazimu kuweko skuli kuendelea na masomo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi madalali na wachuuzi wa samaki katika bandari hizo, wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakishuhudia wimbi kubwa la watoto muda wote wakifanya kazi za uparaji wa samaki.

Mfanya biashara wa samaki Said Ali, alisema kutokana na hali hiyo wakuu wa bandari wanapaswa kuweka mikakati madhubuti ya kuwakataza watoto hao kujiingiza katika bishara hiyo wakati wa muda wa skuli.

Alisema iwapo wasimamizi wa bandari hizo, kama watapiga marufuku hayo na kuzuwia hali hiyo kwa watoto basi watakuwa wamewajengea mustakbali mzuri wa maisha yao vijana hao.

“Suala la elimu ni jambo la muhimu sana, serikali imejitahidi kuwekeza miundombinu mizuri ya elimu, sasa ni wakati kwa jamii kuwahimiza watoto kwenda skuli kusoma na kuachana na ajira za utotoni”alisema.

Asha Omar mwinjuma mchuuzi wa samaki bandari ya Tumbe, aliwataka wazazi na viongozi wa bandari hiyo kusimama kidete kuwaondosha watoto wanaojishuhulisha na biashara hiyo.

“Hapa hakuna siku ya Jumamosi wala siku za kazi, watoto ni wengi katika kujishuhulisha na biashara hizi ili kuwajengea mustakbali mzuri vijana wetu”alisema.

Kizungumzia juu ya suala la ubanjaji wa Kokoto, Amina Chumu Kombo mkaazi wa Micheweni, alisema sababu kubw ainayowafanya watoto kujiingiza katika ajira hizo ni kutokana na baadhi ya familia kuishi katika maisha duni na kupelekea kutokua na fedha za kujikimu kimaisha.

“Kuna baadhi ya watoto hawa wanahudumia familia zao kimaisha, wapo ambao wamekosa baba sasa kama hawakufanya hivyo basi wataishia kulala na njaa”alisema.

Shaban Haji Miwnyi alisema hakuna mzazi ambaye anapenda mtoto wake kuingia katika ajira hizo, baadhi ya watoto ni wakaidi na huduma zote wanapatiwa kwao, bali hutimiza utoto wao na kushindwa kwenda skuli kusoma.

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahaya, akizungumza katika mkutano wakusikiliza kero za wananchishehia ya mjini Wingi, alisema jumla ya wanafunzi elfu saba na mia sita (7600)wa Skuli za Msingi Wilaya ya humo, wamekatisha kuhudhuria masomo yao kutokana na sababu tofauti, ikiwemo ajira za kupara samaki bandarini na kuvunja kokoto.

Mkuu huyo alisema suala la elimu ni jambo la muhimu katika maisha ya watoto, serikali imejenga miundombinu mingi ya elimu kwa lengo la kuwapatia watotio elimu bora.

“Natoa muda hadi mwezi Disemba wanafunzi hao warejshwe Skuli, kinyume cha hapo atawachukulia hatua za kisheria wazazi, ambao watashindwa kutekeleza agizo hilo”alisema.

Alisema haiwezekani wazazi kushindwa na watoto wao, kuwahimiza kwenda skuli kusoma kwani kama kipindi chao wangekuwa kama hivyo basi kusingekuwepo na taifa bora la sasa.

Alifahamisha kuwa haipendezi kumuona mazazi anashindwa kumuhimiza mtoto wake kwenda kusoma na badala yake kumuhamasisha kwenda kubanja kokoto au uparaji wa samaki, jambo ambalo ni kinyume haki ya mtoto.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Omar Issa Kombo aliwataka wazazi kusimamia na kudhibiti utoro huo wa wanafunzi na sio kuwaachia walimu peke yao.

Alisema Wazazi wana wajibu wa kuwahimiza watoto kwenda skuli kusoma, sio kwenda katika shuhuli nyengine, kwani elimu ndio kila kitu katika maisha ya sasa na baadae kwa watoto.

Aidha alifahamisha kwamba Serikali imekua ikiwajibika kwa upande wake, katika kuweka maiundombinu bora na rafiki kwa watoto, kuwepo kwa utoro ni kiutokuitendea haki serikali na ukosefuwa maendeleo.

Naye Afisa Elimu Wilaya ya Micheweni Ismail Ali, aliwataka wazazi ambao watoto wanao wanasoma katika skuli kushirikiana na Serikali kuwatafuta na kuwarejesha skuli watoto waliotoroka Skuli.

“Kijana hata kama alikimbia muda gani, anapaswa kurudi skuli na walimu watampokea na kumuelekeza kwenye muelekeo, ili aweze kufikia malengo yake”alisema.

Hamada Akida Ali mzazi skuli ya shehia ya mjini wingi imejitahidi katika kuwarudisha skuli, kutokana na kufanya kazi kubwa ya kuwarudisha skuli watoto kuendelea na masomo yao.

Mmanga Abdalla haji mkazi wa Wingwi, alisema tatizo ni watoto wenyewe kujiingiza katika biashara hizo, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao ikizingatiwa bado ni wanafunzi.

EMAIL:abdisuleiman33@gmail.com

MWISHO