Monday, January 17

Rais Samia ataka Uganda,Tanzania ziondoe vikwazo vya biashara

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri wanaohusika na masuala ya biashara na uwekezaji wa Tanzania na Uganda wakutane haraka kwenye tume ya pamoja ya ushirikiano waangalie changamoto zilizoainishwa kwenye kongamano la wafanyabiashara ili ziondoshwe.

Hayo yamesemwa leo na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliposhirikiana na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni katika kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda jijini Dar es Salaam,akizitaka pande mbili ziondoe kero zinazokwamisha ushirikiano wa kibiashara.

”Niwaombe tena mkutane mara nyingi na jana tumewataka mawaziri wetu wakutane haraka kwenye ile tume yetu ya pamoja ya ushirikiano waangalie changamoto tulizozizungumza ziondoshwe ili wafanyabiashara muweze kukaa mkijua kuwa serikali imeondosha vikwazo nanyi muondoshe vya kwenu ili muweze kufanya kazi kwa haraka na tuone matokeo ya haraka.”Alisema Rais Samia.

”Makongamano kama haya yaendelee, kwasababu kule nyuma mlikuwa mnavutana serikali huku serikali kule, wafanyabiashara , badala ya kukaa kuangalia vikwazo ni vipi na vipi mnaviondosha mlikuwa mkivikishikilia vikwazo hivyo na kuwekeana ‘kauzibe’ wasije na nyie msiende, hiyo haisaidii upande wa Uganda wala Tanzania, la maana ni kuondoa vikwazo na wote tukasonga mbele.”Aliongeza.

Rais Samia amesema kwamba mipaka iliyopo iliwekwa kwa madhumuni ya utawala lakini serikali ya Tanzania inaweka mipaka mipya ya mabomba ya gesi ya mafuta n.k hivyo amewataka wafanyabiashara wawe huru kwenda huko na kwenda huko kufanya biashara.

”Wafanyabiashara wa Tanzania nyinyi ni mashahidi, tulikuwa tunavutana hapa na Kenya, kila kilichokuwa kinakwenda hakipiti,huku hakipiti na huku hakipiti, kule wakizuia na Mkuu wa Mkoa wetu naye anasema kuanzia leo hakipiti , lakini tulikaa tukaelezana ukweli, tulikuwa tunachomeana kuku mipakani, dhambi tupu viumbe wa Mungu, mnamwaga petroli mnachoma haikuwa na maana,lakini tumeondoa vikwazo na biashara imekuwa mno, ukiangalia figure za biashara Kenya na Tanzania imekua mno, tunataka biashara ikakue upande wa Uganda pia”. Alisema Rais Samia

Rais Samia azitaka Tanzania, Uganda kuondoa vikwazo vya biashara

”Mh. Rais alisema hapa aliomba sisi tukanunue sukari kwake, lakini walisikia kauli za waziri wetu kwamba ‘hatutanunua, hatutakubali’, that was nonsense, Mh. Rais tutanunua sukari kutoka Uganda.”

Kongamano la wafanyabiashara limelenga katika kuzungumzia fursa za biashara ya mafuta na gesi hususani maendeleo ya mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni

CHANZO CHA PICHA,IKULU TANZANIA

Rais Samia amesema kuwa Serikali ya Uganda imeiunga mkono serikali ya Tanzania katika mambo muhimu ambayo yamesaidia katika maendeleo ya mradi wa bomba la kusafirisha mafuta. Kufuatia hatua hiyo, Rais Samia ametoa wito kwa wataalamu wa Tanzania na Uganda kuangalia masuala muhimu yatakayowezesha kuleta ushirikiano katika sekta ya mradi huo.

”Nchi zetu zimejaaliwa kuwa na rasilimali au maliasili nyingi ambazo hazijatumika ipasavyo, kwa madhumuni ya kukuza uwekezaji, hivyo basi ni muhimu kuendelea kuvutia uwekezaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda vinavyotumia malighafi za ndani hususani kwenye sekta za kilimo, na maliasili, viwanda vinavyotumia nguvu kazi zaidi ili kuzalisha ajira, viwanda vinavyoendana na ukuaji wa miji, viwanda vitakavyozalisha bidhaa kukidhi mazingira ya biashara na kuwekeza zaidi kwenye rasilimali watu. Na viwanda vinavyozaa viwanda vingine, kama vya mbolea na kemikali”.

Rais Samia amesema kwamba serikali ya Tanzania imefanya maboresho kadha wa kadha ili kuvutia uwekezaji ikiwemo kupunguza muda wa upatikanaji wa vibali vya kazi kwa kuondoa urasimu ambapo hivi sasa, hata ndani ya siku moja mwombaji anaweza kupatiwa kibali kwa mfumo wa kielektroniki, tofauti na wakati uliopita vibali vilikuwa vinachukua miezi sita au hata zaidi.

CHANZO NI BBC/SWAHILI