Sunday, June 26

Milele Zanzibar Foundation yatoa msaada kwa wanafunzi wa Skuli ya Utaani na Chasasa.

 

NA HANIFA SALIM.

TAASISI ya Milele Zanzibar Foundation, imetoa msaada wa vifaa kwa manusura waliopata na janga la moto katika skuli ya sekondari Utaani na Chasasa Wete vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 20.

Msaada uliotolewa kwa wanafunzi hao ni mikoba 404, kanga 481, viatu 500 na wino nne za fotokopi kufuatia kwa janga la moto liliopelekea kuungua kwa nyumba wanayolala wanafunzi wa kike (dahalia) mwezi machi mwaka huu.

Akikabidhi msaada huo Meneja wa taasisi ya milele Zanzibar Foundation Pemba Abdalla Said Abdalla alisema, fedha hizo ambazo zimetolewa ni ahadi walioiweka mara tu baada ya kutokea janga la moto kwenye skuli hiyo.

Alisema, hatua zinazochukuliwa na milele ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi dk. Hussein Ali Mwinyi za kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira salama.

“Moja kati ya masharti yetu milele hatutoi fedha tunachokitoa ni vifaa vyenye thamani ya fedha lakini lengo letu ni kuwafikia walengwa haya ni katika maadili na sheria za milele,” alisema.

Hata hivyo alisema, serikali yao inaendelea kutafuta vyanzo vya majanga hayo kwani sasa yamekua yakijitokeza siku hadi siku, hivyo aliwataka wanafuzi kuacha kutumia vyombo vya umeme bila ya kufuata utaratibu ili kuepusha matukio hatarishi.

Afisa elimu Mkoa wa Kaskazini Pemba Khamis Said Hamad alisema, milele ni taasisi ambayo inajitahidi sana kuisaidia sekta ya elimu nchini ili kuhakikisha inapiga hatua za kimaendeleo.

“Milele tunawashukuru kwa moyo wenu wa uzalendo na upendo wa dhati kwetu kwani akufae kwa dhiki ndie wako rafiki, wanafunzi nataka mutambue miongoni mwa rafiki wema kwenu ni milele,” alisema.

Aidha alisema, taasisi ya milele ndio watu wa mwanzo kujitokeza kuwafariji mara tu baada ya kutokea kwa janga hilo, ambapo hadi leo faraja yao inaendelea kwao.

Hata hivyo aliwataka milele waendelee kuwasaidia hata kwa jengo lao ambalo limeungua kwani alisema, kuungua kwa jengo hilo ni changamoto kubwa ambayo kwa sasa inawalazimu wanafunzi kulala katika vyumba vya kusomea.

Mwanafunzi wa skuli ya sekondari Utaani Afea Ame Busra, ameishukuru taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kwa msaada ambao wamewapatia na kuwaomba isiwe mwisho kuwasaidia.

Kwa upande wake mwanafunzi wa skuli ya sekondari Chasasa Amina Mtata Yahya alisema, milele imejitokeza tangu mwanzo lilipotokea janga la moto kwenye skuli yao hadi sasa ni jambo la kujivunia uwepo wao.

                                      MWISHO.