Thursday, August 11

MWANAHARAKATI awataka waandishi kuisemea sheria ya habari

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MTAALAMU wa Uchambuzi wa Sheria kwenye mradi kuhamasisha Mabadiliko ya
Sheria ya Habari Zanzibar Hawra Mohamed Shamte alisema, kuna haja kwa
waandishi wa habari kuisemea sheria yao kutokana na kuwa ni ya zamani
na baadhi ya vifungu ni kandamizi kwao.

Akiwasilisha sheria ya Wakala wa Habari, magazeti na vitabu pamoja na
sheria ya Tume ya Utangazaji mchambuzi huyo alisema kuwa, sheria
iliyopo ni ya tangu mwaka 1980 ambapo baadhi ya vifungu huwakwaza
waandishi wa habari.

Alisema kuwa, ni wakati sasa kwa waandishi kuisemea sheria hiyo ili
iweze kufanyiwa maboresho, kwani kufanya hivyo ni kupigania uhuru wa
kujieleza na kutoa maoni ambayo ni haki ya msingi ya binaadamu na ndio
msingi wa maendeleo ya jamii yeyote ulimwenguni.

“Ni kwa miaka 12 sasa harakati za kupigania uwepo wa sheria nzuri za
habari zinafanyika kwa maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla, hivyo ni
wakati sasa kwa waandishi hao kupaza sauti zao ili tuone kwamba
tunafanikiwa katika hili”, alieleza.

Kwa upande wake mwezeshaji Shifaa Said Hassan alisema kuwa, ni muhimu
sana kuzieleza sheria na mapungufu yake katika vyombo vya habari,
kwani tangu mwaka 2010 wamekuwa wakiorodhesha mapungufu yaliyomo,
ingawa bado inaendelea kutumika sheria hiyo hiyo.

“Kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anazifanyia utetezi sheria hizi
kwenye vyombo vyao vya habari, tuvichambue vifungu ambavyo vinatunyima
uhuru, tutakapofanya hivyo itakuwa tumeisaidia jamii yetu”, alisema
Shifaa.

Mapema akifungua mafunzo hayo Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa
Said alisema, mradi wa kuhamasisha mabadiliko ya sheria ya habari ni
wa miaka minne, ambapo aliwataka wanahabari kuchukua juhudi mbali
mbali ya kuzisemea sheria hizo ambazo zinawakwaza kwa lengo la
kuboresha tasnia ya habari nchini.

Nae Mratibu wa mradi huo Mohamed Khamis alisema, watashirikiana na
wanahabari kwa ajili ya kuongeza nguvu, ili kupata sheria bora za
habari.

“Kwa miaka kadhaa wadau wanakutana na kuichambua sheria hii na kutoa
mapendekezo yao, ingawa bado kuna baadhi ya vifungu vinakandamiza
uhuru wa habari”, alieleza.

Akichangia katika mafunzo hayo mwandishi kutoka mtandao wa Pemba
today, Haji Nassor Mohamed alipendekeza kwamba  ikiwa mwandishi ama
vyombo vya habari vimetuhumiwa kutenda kosa visifungiwe hadi pale
yatakapotoka maamuzi ya mahakama.

“Hii inaumiza sana kwa sababu wanakosa kazi na biashara inasimama,
vyombo vya habari husimamishwa kazi kabla kesi hazijafika mahakama,
hivyo tunaomba kuwepo kifungu cha kuendelea na kazi mpaka pale kesi
itakapomalizika kama ilivyo kwa kesi nyengine”, alisema.

Mwandishi wa habari wa Radio Jamii Micheweni Time Khamis Mwinyi
aliipongeza TAMWA pamoja na MCT kwa juhudi zao za kuwaelewesha
wanahabari sheria yao, kwani kuna baadhi ya vifungu vimekuwa
vikikwamisha maendeleo ya habari, ingawa walikuwa hawajui.

Mafunzo hayo ya siku moja ya kuhamasisha mabadiliko ya sheria ya
habari yalifanyika katika Ukumbi wa TAMWA Mkanjuni Chake Chake, ambapo
walihudhuria waandishi wa vyombo mbali mbali kisiwani hapa.

MWISHO.