Friday, September 29

RC Mattar akutana na wakuu wa taasisi za serikali pemba, juu ya uhamasishaji ukusanyaji wa kodi kwa kutumia risiti za kieletroniki

MKURUGENZI wa ZRB Pemba Jamal Hassan Jamal, akifungua mkutano wa uhamasishaji wa kodi kwa watendaji wa wakuu wa serikali Kisiwani Pemba, mkutano uliofanyika katika ofisi za ZRB Pemba huko Gombani Chake Chake.
BAADHI ya wakuu wa Wilaya, makatibu Tawala na maafisa wadhamini Pemba, wakifuatilia kwa makini mkutano wa uhamaishaji wa Kodi kwa watendaji wa Serikali, mkutano uliofanyika Ofisi za ZRB Gombani.
AFISA Mdhamini Ofisi yay a Rais Fedha na Mipango Pemba Abdulwahab Said Bakar, akizungumza katika mkutano wa uhamasishaji wa Kodi kwa watendaji wa Serikali, mkutano uliofanyika Ofisi za ZRB Gombani.
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Masoud, akizungumza na watendaji wa kuu wa Serikali Kisiwani Pemba, juu ya suala la uhamasishaji wa kodi kwa watendaji hao, mkutano huo uliofanyika katika ofisi za ZRB Gombani.
AFISA Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, akichangia katika mkutano wa uhamasishaji juu ya ukusanyaji wa Kodi,kwa watendaji wa wakuu wa serikali Pemba.

BAKAR MUSSA-PEMBA.

WATENDAJI wakuu wa Serikali kisiwani Pemba , wametakiwa kuondowa
muhali na kuweka mbele uzalendo wa nchi yao katika usimamizi wa kodikupitia mashine za Elektronik EFD.

Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud alieleza hayo huko katika ukumbi wa Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) ulioko Gombani Kisiwani humo wakiwemo Wakuu wa wilaya , kamati ya ulinzi na Usalama na wadau mbali mbali.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia ZRB imejipanga kukusanya mapato kwa kutumia mashine hizo ili kuwa na uhakika wa mapato hayo kufika Serikalini kwa kuwapatia wafanyabiashara mashine hizo lakini matumizi yake yamekuwa yakisusua ni mdogo.

Alieleza kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mipango yake ya maendeleo kwa wananchi wake kwa kutumia kodi zinazolipwa na wananchi kupitia biashara wanazozifanya , hivyo ni lazima wananchi waondokane na mazoweza ya kudai na kutoa risiti pale wanapofanya miamala.

“Huduma zinazotolewa na Serikali katika sekta tafauti zinatokana na uwepo wa fedha za kutosha kama vile bara bara, afya , ulinzi n,k hivyo ulipaji kodi kwa hiari ni jambo la Uzalendo”, alisema RC.

Mattar ,alisema Serikali inategemea kodi za ndani ili zisaidie kwa matumizi yake badala ya kutegemea wafadhili na hilo haliwezi kufikiwa iwapo kila mmoja hatokuwa tayari kusimamia na kuhamasisha kutowa na kudari risiti pale wanapofanya miamala mbali mbali.

Alifahamisha kuwa ni wajibu wakila kiongozi kuhamasisha kulipa kodi kwa hiari kama ni haki kwao  kwani hata wafadhili ambao wamaekuwa wakiisadia Serikali wameathiriwa kwa changamoto mbali mbali ikiwemo vita na ugonjwa wa Covid 19.

Alisema kitakacholeta ujasiri kwa Serikali katika harakati za
maendeleo kwa wananchi wake ni kuhakikisha kila mmoja anatekeleza wajibu wake kwa kulipakodi anayostahili.

Mkuu wa mkoa huyo alieleza usimamizi wa sio kazi ya  Bodi ya mapato pekee , kila mmoja kazi hiyo inamuhusu hivyo viongozi waondowe muhali kwa kuhoji wananchi juu ya risiti za bidhaa wanazouza ama kununuwa.

“Pamoja na msisitizo wa Rais na viongozi mbali mbali juu ya kuwataka wananchi wakiwemo wafanyabiashara kulipa kodi kwa kutumia mashine za EFD lakini suala la utowaji risiti ni mdogo pamoja na kufanyika miamala ya manunuzi siku hadi siku”, alieleza.

Aliwataka wasimamizi wakodi kutokuwa na matumizi ya nguvu katika kudai kodi ipokuwa wasimamiwe na wahamasishwe kutowa na kudai risiti ya Elektronik na sio ya mkono sambamba na kuhakikisha kila mmoja anayo mashine ya kutolea risiti na anaitumia.

Alisema kulipa kodi ni kwa ajili ya maslahi ya nchi lakini kuna baadhi ya walipakodi wakiwemo Wafanyabiashara sio waaminifu na hatimae wanalipa kodi pungufu pamoja na kumiliki mitaji mikubwa.

Alifahamisha kuwa ni vyema kutumia hekma na busara katika kudai kodi ili kujenga uhusiano mwema baina ya Serikali na walipakodi badala ya kutengeneza uadui kwa wakusanya kodi na wafanyabiashara.

“Musiwatishe sana wafanyabiashara munapokwenda kukusanya kodi lakini lazima wahakikishe kila alie na wajibu wa kulipa kodi anafanya hivyo ili mwananchi apate na Serikali ipate mapato yake kihalali”, alieleza.

Alisema ni vizuri kuweko mkakati maalumu wa kusimamia kodi sambamba na kufanyika mipango ya kuondowa utitiri wa kodi ili kuwaondolea malalamiko walipakodi ambayo wamekuwa akiyatowa siku hadi siku.

Aliwataka watendaji wa Serikali kuendelea kuwa mfano wa kulipa kodi kwani kodi ya zuwio ( with hollding tax) hali sio mzuri na yoyote ambae hatotekeleza wajibu wake Serikali haitomuonea haya wala muhali.

Kwa upande wake Ofisa mdhamini wizara ya fedha na mipango Pemba,
Abdulwahab Said Bakar alieleza kuwa Serikali imepanga kukusanya mapato kiasi ya Tsh, bilion 2.59 kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023  ambapo ni ongezeko la asilimia 40 ya bajeti iliopata ya mwaka 2021/2022 .

Alifahamisha kuwa asilimia 53 ya makusanyo hayo inategemea mapato ya ndani na hilo haliwezi kutekelezeka iwapoa hakutokuwa na mashirikiano baina ya Viongozi wa taasisi za Serikali na wadau mbali mbali wa kodi.

“ Viongozi wenzangu naomba tushirikiane kwa pamoja ili tuweze kufikia malengo ya Serikali kuhusiana na makusanyo hayo ya mapato ya Serikali”, alieleza.

Nae meneja wa ZRB Pemba Jamal Hassan Jamal aliwataka wananchi na
wafanyabiashara kisiwani Pemba kuhakikisha kila mmoja anawajibu wa kulipia kodi inayomuhusu kwa kuwa tayari kudai na kutowa risiti anapouza ama kununuwa.

Aliwahamiza wananchi kukataa risiti ya mkono pale wanapofanya manunuzi na wawe tayari kudai risiti ya Elektronik kwani ndio Serikali inavyotaka.

Nao washiriki wa mkutano huo waliiomba Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) kutafuta mbinu zaidi za uhamasishaji kwa kutumia michezo,
mihadhara,hotuba kwa viongozi wa dini, ili kufikisha ujumbe wa kodi kwa urahisi kwa wananchi.

Hata hivyo walisema ni vyema kuundwa kamati maalumu ya kufauatilia namna ya ukusanyaji wa mapoto kwa kutumia  risiti za Elektronik na wananchi walivyo na muamko wa kudai risiti hizo.

MWISHO.