Saturday, May 18

Bandari ya Wete yapokea meli ya MV Zahra II ikiwa na kontena 42 za mchele na sukari zikitokea Mombasa .

NA ABDI SULEIMAN.

MELI ya Mizigo MV ZAHRA II iliyobeba kontena 42 zilizokuwa na shehena ya Mchele na Sukari, zikitokea bandari ya Mombasa nchini Kenya, imeweza kufunga gati katika bandari ya Wete na kuteremsha bidhaa hizo za mfanyabiashara Ali Shaib Ali.

Kuwasili kwa meli hiyo ni kungua njia kwa baadhi ya wafanya biashara kuona sasa ipo haja ya mizigo yao kutoka nche ya nchi kuiteremsha moja kwamoja katika kisiwa cha Pemba kwa kutumia bandari ya Wete na Mkoani.

Akizungumza na waandishi wa habari huko bandarini Wete, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya shirika la Bandari Zanzibar Joseph Abdalla Meza, wakati waziara ya bodi hiyo kukagua maeneo ya shirika Bandari Tawi la Pemba.

Alisema ujio wa meli hiyo ni ishara ya Kisiwa cha Pemba kuanza kufungua katika suala zima la uwekezaji, kupitia bandari zilizopo ndani ya kisiwa hicho.

Alifahamisha kwamba sasa meli ndogo ndogo zinaweza kushusha mizigo katika bandari mbali mbali, changamoto ni kutokuwepo kwa vifaa vya kutosha vya kubebea konta zinapofika katika meli.

“Bodi imefika na imeona changamoto hiyo itakwenda kuzifanyia kazi, ili meli zinazokuja Wete nazo ziweze kususha hata kontena na kuwepo na sehemu maalumu ya kuzihifadhi kama itakavyokuwa kwa upande wa mkoani,”alisema.

Alisema kwa sasa bandari ya Wete wanakwenda vizuri, tayari meli za Kontena zinawasili na zinafungulia ndani ya meli hiyo na watu wanashusha mizigo yao na ndani ya Meli hiyo moja kwa moja.

Aidha aliwataka wafanyabishara baada ya kwenda Unguja kushusha mizigo yao, badala yake ni kuileta Pemba moja kwa moja na kuishusha kwa lengo la kupunguza gharama.

“Ili kupunguza gharama kontena ikiwasili Mombasa au dar, vizuri mzigo ukaja ukaufungulia Pemba moja kwa moja hapo itakuwa umepunguza gharama za mzigo wako na sio kuufungulia huko,”alisema.

Hata hivyo alisema iwapo wafanyabiashara kama watafanya hivyo,  wataizindua Serikali kuweza kuziboresha zaidi bandari hizo, pia ni njia moja ya kupunguza mzigo katika bandari ya Unguja.

Naye Mkurugenzi shirika la bandari Tawi la Pemba Abdallah Salim Abdallah, alisema ni kawaida kwa kila miezi miwili kupokea meli kubwa za kontena kama hizo na kuteremsha mizigo moja kw amoja kutoka ndani ya meli.

“Mwelekeo mpya wa bandari ya Wete ni kuhakikisha huduma zinatolewa pale kama sheria za kimataifa zinavyotaka, huduma zitaboreka na uingizaji wa meli za mizigo zitaongezeka,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wafanyabiashara kukubaliana na kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi, juu ya kukifungua kisiwa cha Pemba kibiasha na kunyanyua uchumi wa Taifa, kwa kuleta meli moja kwa moja ndani ya kiswa hicho na kuteremsha mizigo yao.

MWISHO