Thursday, June 13

“Serikali kuwapatia kifuta jasho wajumbe wakamati za Jamii za Shehia kwa kazi kubwa wanazozifanya”MKURUGENZI PEGAO

NA ABDI SULEIMAN.

MKURUGENZI Mradi wa SWIL kutoka PEGAO Hafidh Abdi Said, amesema wakati umefika kwa wajumbe wakamati za Jamii za Shehia kutoka Wilaya Nne za Pemba, kuhakikisha zinapatiwa kifuta jasho serikalini kutokana na kazi kubwa wanazozifanya za kufatilia changamoto za shehia na kuweza kutatuliwa.

Alisema kamati hizo zinafanya kazi ambazo zilipaswa kufanya na viongozi wa majimbo, Wilaya hata baadhi ya watendaji wa serikali, kwa lengo la kuwasaidia wananchi.

Mkurugenzi huyo aliyaeleza hayo katika kikao kilichowakutanisha wajumbe wa kamati hizo, cha kuwasilisha ripoti zao za utekelezaji kupitia mradi wa SWIL kikao kilichofanyika Mjini Chake Chake.

Alisema katika utekelezaji wa mradi huo, Pemba inaweza kuwa ya mfano kutokana na kazi zake kufanya kwa umakini na ufuatiliaji wa hali ya juu.

“Hata mradi ukamalizika lazima tufahamu kwamba kamati zitaendelea kufanya kazi zake kwa jamii, hizi kamati zipo kusaidia jamii na sio PEGAO,”alisema.

Hata hivyo aliwataka akinababa kuhakikisha wanawapa nafasi akinamama, wakati watakapoanza harakati za kuwania upongozi lengo ni kuona akinamama nao wanashiriki katika masuala ya kimaendeleo.

Naye mratibu wa mradi wa kuwawezesha wanawake katika nafasi za uongozi(SWIL) Dina Juma, alisema kikao kilichopita walipeana mafunzo na kujengea na uwezo, jinsi ya kufuatilia changamoto za zinazowakabili katika shehia zao baada ya kuziibua.

Kwa upande wake afisa kutoka TAMWA Pemba Asha Mussa Omar, aliwakumbusha wanakamati hao kuhakikisha wanawanahamasisha na wanawaume kushiriki katika masuala mbali mbali.

Wakiwasilisha ripoti zao baadhi ya viongozi wa kamati hizo, wamesema wamepata mafanikio makubwa baada ya kuibua changamoto na kuzifuatilia mwisho wa siku zimeweza kutatauliwa.

Hidaya Omar Juma kutoka shehi ya Mjananza, ameweza kuibua watoto watoro 30 wanawake sita na wanaume 24, ambapo wanafunzi 27 wamejiunga na elimu mbadala wanaume 24 na wanawake watatu, huku 17 wakiendelea na elimu mbadala na watatu wamefaulu mchipuo mwaka huu.

Naye Mize Mbwana Hassan kutoka shehia ya Mpambani Kojani, alisema changamoto ya maji ndio tatizo kwao huku waathirika wakiwa ni wanawake na watoto zaidi ya 200.

Alisema maji hufuatilia zaidi muda wa usiku, hali inayopelekea baadhi ya watoto kukosa kwenda skuli ikizingatiwa kojani ni kisiwa kilichozungukwa na bahari.

“Sisi viongozi wa kamati tulipoambiwa tumeambiwa miundombinu ni ya kizamani, mashine pia ni ndogo kiuchumla hali ya maji kojani haiku vizuri,”alisema.

Alisema changamoto nyengine ni elimu, ambapo zaidi ya wanawake 100 kojani hawajuwi kusoma na kuandika, tayari wameshaomba kuanzisha madarasa matano ya wanakisomo cha watu wazima.

Kwa upande wa shehia ya Shanake na Kiuyu Mbuyuni, waliishukuru serikali kwa jitihada wanawazozifanya katika kutatua changamoto za jamii katika maeneo mbali mbali.

MWISHO