Saturday, January 18

WAFUGAJI samaki Pemba wataka Mahakama yao

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

WAFUGAJI wa Samaki Kisiwani Pemba wamesema wakati umefika sasa na wao kuwa na mahakama yao maalumu, itakayoweza kuwatia hatiani wizi wanaoiba samaki kwenye mabwawa.

Walisema mahakama zilizopo hivi sasa, mahakimu hawajuwi uchungu na ugumu wanaoupata wafugaji wa samaki, hali inayopelekea watuhumiwa wa wizi wa samaki kuchanganywa na watuhumiwa wengine na adhabu zinazotolewa hakizi haja.

Waliyaeleza hayo wakati wakichangia mada mbali mbali zilizowasilishwa, katika mafunzo ya ufugaji wa samaki wa Mwatiko, yaliotolewa na taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na maliasili za Baharini, kupitia mradi wa kuendeleza kilimo na uvuvi (AFDP) na kufanyika Chake Chake.

Mmoja ya wafugaji wa Samaki Adam Mohamed Abeid, alisema wafugaji wa samaki wamechoka kuibiwa samaki wanaofuga, huku wizi baada ya siku mbili wanadunda mitaani.

“Leo unatengeneza bawa na hadi kutia samaki linaweza kukugharimu Milioni 20, unampeleka mwizi mahakamani hakimu anakuuzi huyo samaki walioibiwa bado wapo hai na wanaukubwa gani au ndio hawa vibua, wakati wemngine wanatia uchungu kutokana na kutokujua ugumu tunaoupata,”alisema.

Alisema hakuna hakimu hata mmoja ambaye atakua na uchungu juu ya ufugaji wa samaki wakati, hakuna hasara wala shida anayopata yeye, hivyo wapo wafugaji wa samaki ambao wamesoma sharia.

Nae Msabah Hamad Khamis alisema wafugaji wa samaki nao wanahitaji sasa kupatia vifaa kama ilivyo wavuvi na wakulima wa mwani, ili kuwasaidia kufanya doria pamoja na kuwasaidia katika ufugaji bora na wakisasa.

Alisem wafugaji wa samaki Zanzibar wananafasi kubwa katika suala la ufugaji wa samaki, iwapo watajikiza katika ufugaji wa kisasa ambao utawapatia tija haraka.

Alisema zipo nchi za jirani zinahitaji samaki, hivyo wafugaji wanapaswa kuchangamkia masoko hayo na kuona kazi ya ufugaji wa samaki ni kama kazi nyengine inayoweza kumpatia kipato na ajira kwao.

“Serikali ilipotangaza itatoa ajira ndio ajira kama hizo, wapo wanaopatiwa vifaa vya uvuvi na serikali vijana wanajiajiri wenyewe, huko ndiko ziliko ajira vijana wanapaswa kufahamu,”alisema.

Kwa upnade wake mfungaji mwegine Khamis Hamad Nassor, alisema biashara ya ufugaji wa samaki ni kubwa na inagharama kubwa, hivyo wafugaji wadogo wadogo wanakazi ya kufikia mafanikio.

Alisema changamoto kubwa kwa wafugaji wa samaki ni suala la wizi, bado wizi wanawarudisha nyuma kufikia ndoto na mafanikio yao katika kazi hizo.

Mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya Uvuvi Zanzibar Dr.Salum Soud, alisema serikali inajitahidi kutafuta wafadhili kusaidia katika masuala mbali mbali ya ufugaji wa samaki ili wafugaji waweze kutimiza ndoto zao.

Mapema Naibu katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Khamis Suleiman Shibu, alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi anashauku sana kuona dhana ya uchumi wa buluu inafanya kazi hali inayopelekea kutumia nguvu nyina katika eneo hilo.

Alisema nia itaendelea kubakia ilele ya kuhakikisha wanapata vifaa na kujitegemea na kupata kipato cha kuendelesha familia zao.

“Hata taifa nalo linakua ni taiafa zuri lenye watu ambao wanaweza kufanya kazi na kujitegemea, na kupata kipato cha kuedesha familia,”alisema.

Kwa upande wake mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili baharini Dr.Zakaria Khamis Ali, alisema tayari mtambo wa uzalishaji wa chakula umeshafika, kwani serikali imejinga kuhakikisha mambo yanakua sawa.

MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper/habari Portal
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355