Thursday, June 13

ASASI ZA KIRAIYA ZINAZOSHIRIKI MAPAMBANO DHIDI YA MAGONJWA YA KIFUA KIKUU ZIMETAKIWA KUONGEZA MASHIRIKIANO

 

Dr. Khalfan Salim Said Mratib kitengo shirikishi Ukimwi, TB, Ukoma na homa ya Ini Mkoa wa Kaskazini Pemba.

NA KHADIJA  KOMBO.

Asasi za kiraya zinazoshiriki katika mapambano dhidi ya magonjwa ya Kifua kikuu wametakiwa kuongeza mashirikiano na kitengo shirikishi cha Ukimwi kifua kikuu , ukoma na homa ya Ini   katika  kuhakikisha wanaibua wagonjwa wengi na kupatiwa matibabu kwa haraka ili  kuepuka  maambukizi zaidi kwa jamii.

Akizungumza na wana Asasi hao katika mkutano wa mrejesho (FEED BACK MEETING )   Mratib wa Kitengo hicho katika Mkoa wa kaskazini Pemba Dr. Khalfan Salim Said   huko katika Ofisi za kitengo hicho Machomanne Chake Chake  Pemba  amesema  kuwa bado  ugonjwa huo upo na juhudi zaidi zinahitajika ili kuutokomeza kabisaa ugonjwa huo.

Akizungumzia kuhusu lengo la Mkutano huo amesema ni kuangalia namna utekelezaji wa kazi hio unavyo endelea pamoja na kuona  mapungufu yaliopo ili yaweze kufanyiwa marekebisho  hivyo amewataka wanaasasi hao kuhakikisha   wanayafanyia kazi  mapungufu yote yanayojitokeza huku wakiongeza   bidi kwa kuibua angalau wagonjwa watatu kwa kila  mjumbe ndani ya jumuiya,  kwa  kipindi cha mwezi mmoja ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.

Kwa upande  wake bi Mwana Bashir kutoka kitengo shirikishi Zanzibar amewataka wana Asasi hao kuhakikisha wanajaza vyema fomu za wahisiwa na wagonjwa  ikiwa ni pamoja na fomu nambari 13a huku wakijenga utaratibu wa kufanya mikutano ndani ya jumuiya zao kwa kila mwezi ili kutathimini utendaji wao na kuangalia namna ya kuongeza bidii katika mapambano hayo.

Akifunga Mkutano huo Mratib wa kitengo hicho kwa Upande wa Kisiwani Pemba Dr. Khamis Hamad amewasisitiza wanaasasi hao kuhakikisha wanatuma ripoti za utekelezaji kwa wakati huku wakimshirikisha Afisa kutoka kitengo hicho kila wanapo fanya mikutano yao.

Dr. Khamis Hamad Mratib Kitengo shirikishi Ukimwi TB Ukoma na homa ya Ini Pemba

Kwa upande wao wana Asasi hao wameaahidi kuyafanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza katika tathmini hio huku wakiomba kupatiwa vitendea kazi vikiwemo vipeperushi ili kusaidia katika kutoa elimu ndani ya jamii.

Mradi wa mapambano dhidi ya kifua kikuu  Zanzibar unaendeshwa  na Wizara ya Afya Zanzibar  kupitia  kitengo shirikishi kifua kikuu ukimwi ukoma na  homa ya ini   pamoja na  asasi za kiraiya chini ya ufadhili wa global fund.

Asasi zinazoshiriki katika mapambano  hayo kwa upande wa Kisiwani Pemba,  ni Pamoja na PEMBA PRESS CLUB, MKUPE JUKAMKU NA  ZANABU.

 

MWISHO.