Tuesday, October 15

ZSTC YAWATAKA WANANCHI KUACHA KUNUNUA, KUUZA KARAFUU KINYUME NA UTARATIBU

NA HANIFA SALIM, PEMBA

MKURUGENZI Mwendeshaji wa shirika la taifa la Biashara la (ZSTC) Soud Said Ali, amewataka wananchi kuacha mara moja suala la ununuaji wa karafuu mitaani, kwani ZSTC haijalala na itamchukulia hatua mtu yoyote atakaebanika. 

Aliyasema hayo huko ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake, alipokua akingumza na waandishi wa habari kufuatia shirika hilo, kukamata karafuu ambazo zimenunuliwa kutoka kwa wananchi katika eneo la Mgagadu Wilaya ya Mkoani Pemba.

Alisema, watu ambao wananunua karafuu mitaani hawajapewa dhamana hiyo bali wanafanya kwa dhumuni la kuhujumu uchumi hivyo, aliwataka wananchi wafahamu kwamba serikali iko macho na vyombo vyake vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya doria kwa kipindi chote cha msiku huu wa zao la karafuu.

“Katika ziara yetu ya kuwatembelea wakulima wa zao la karafuu kwenye mashamba na kambi zao msimu huu, tumegundua watu ambao wanapita kuwadhulumu wakulima, wananunua karafuu kwa pishi tofauti na ambazo zinatumiwa na ZSTC”, alisema.

Alieleza, ZSTC katika maandalizi yake ya msimu wa karafuu mwaka 2024-2025, imebaini mambo ambayo hayapo sawa ya kuhatarisha uwepo wa zao hilo na uchumi wa nchi, ikiwemo watu kupita mitaani kununua karafuu kwa bei ya chini na kutumia pishi zenye ujazo tofauti.

Aidha aliwataka, wananchi kuwafichua na kuwaripoti watu ambao wananunua karafuu mitaani kwa shirika la taifa la Biashara ZSTC ili kuona wanachukuliwa hatua sambamba na kuziuza karafuu zao katika vituo vilivyowekwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ZSTC Pemba Abdalla Ali Ussi alisema, ununuzi wa karafuu kwa wakulima ni kitendo ambacho kinalaaniwa na shirika hilo, kwani serikali imeipa jukumu ZSTC pekee na ndio mwenye mamlaka ya kufanya hivo.

Hata hivyo, aliwaomba wakulima wa zao hilo waitikie wito wa serikali wa kwenda kuziuza karafuu hizo kwenye vituo vilivyowekwa kwa mujibu wa utaratibu pamoja na kujiepusha na magendo kwani alisema, endapo utapatikana hukumu zake ni kubwa.

MWISHO.