Tuesday, November 12

SMZ KUHAKIKISHA WALIMU WANAPATIWA MAFUNZO WAKIWA KAZINI

ZANZIBAR

Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar itaendelea kuhakikisha walimu wanapata mafunzo wakiwa kazini yatakayowasaidia kuongeza ujuzi wa hali ya juu ambao utawasaidia katika kutekeleza mfumo mpya wa elimu.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Walimi Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema ni jambo la muhimu sana kufanyika kwa Maadhimisho ya siku ya walimu duniani yanayolenga kutathmini mafanikio na changamoto za walimu katika kufikia mapendekezo ya hadhi ya walimu yaliyowekwa na UNESCO na ILO yanayosisitiza Taaluma, mazingira bora, hadhi, heshima na maslahi ya walimu.

Mhe.Hemed amesema Serikali katika kulinda hadhi na maslahi ya walimu imeanzisha Tume ya Utumishi ya walimu ambayo madhumuni yake ni kusimamia ustawi na kuendeleza kutunza heshima ya walimu pamoja na kusimamia ujenzi wa makaazi ya walimu na dahalia za wanafunzi katika skuli mbali mbali Unguja na Pemba.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa Serikali imekusudia kujenga chuo cha Uwalimu ambacho kitatumika kutoa mafunzo kwa walimu na kuwajengea uwezo unaoendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknoloji duniani ili waweze kufundisha kwa ufanisi zaidi.

Sambamba na hilo Makamu wa Pili wa Rais amewataka walimu kuitumia vyema fursa ya kukusanyika pamoja kwa kubadilishana uzoefu na maarifa na kuliwekea msisitizo suala la uwajibikaji kazini, maadili mema kwa walimu na wanafunzi na kukumbusha sifa za mwalimu bora hasa katika kipindi hiki ambacho Zanzibar inafanya maguzi makubwa ya Mfumo wa elimu.

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza kuwa serikali kwa kushirikiana na wizara ya elimu na mafunzo ya amali itahakikisha inazitatua changamoto zote zinazowakabili walimu ikiwemo malimbikizo ya fedha za likizo na ufiwa.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mohamed Mussa amesema walimu wana jukumu la kujiongeza kitaaluma na kujiendeleza kielimu kwa walimu wa ngazi zote ili kuendana na mageuzi ya mfumo wa elimu ambao unatumia zaidi Teknolojia na kuwafanya walimu waendane na matakwa ya elimu duniani.

Mhe. Lela amesema kwa kuhakikisha sekta ya elimu inazidi kuimarika Wizara ya elimu imekuwa ikikutana na Uwongizi wa chama cha wafanyakazi na chama cha walimu ili kujadili maslahi na ustawi wa walimu na sekta ya elimu kwa ujumla.

Amesema kuna changamoto nyingi zimejitokeza baada ya ugatuzi ikiwemo posho na nauli za walimu jambo ambalo lipo katika hatua za mwisho za utekelezaji wake na kuwaahidi walimu kuwa Serikali kupitia Wizara ya elimu itahakikisha maslahi na haki za walimu zinapatikana kwa wakati.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Zanzibar ( ZATU ) Mwalimu HAJI JUMA amesema siki ya walimu duniani inatoa fursa kwa walimu kutafakari mafanikio na changamoto katika sekta ya elimu hasa katika kuinua viwango vya elimu na ustawi bora wa walimu na wanafunzi nchini.

Mwalimu HAJI ameiomba Serikali kuangalia umuhimu wa kuwashirikisha walimu ipasavyo hasa katika ngazi za maamuzi ili kuzidi kuiimarisha sekta ya elimu kwa kutoa elimu bora kwa wanafunzi wote wa Zanzibar.

Amesema ili kuendelea kuboresha sekta ya elimu na mazingira ya utowaji wa elimu bora nchini jitihada za pamoja zinahitajika kati ya Serikali, walimu na wazazi ili kutoa matokeo chanya ya ufaulu kwa wanafunzi wa Zanzibar.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR)
Leo …tarehe 05 / 10 / 2024.