NA ABDI SULEIMAN.
MRATIBU wa Wakala Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA)Afisi ya Pemba, Haji Mohd Haji amesema katika kipindi cha Miaka minne ya Uongozi wa Dkt.Hussein Ali Mwinyi, fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi zimeimarika Zanzibar, kwani ZEEA inazungumzia bilioni 31.8 kwa wanufaika zaidi ya elfu 21.
Alisema fedha hizo kwenye program ya Inuka, program ya 4.4.2 ambayo imeanza kazi mwaka huu wa fedha na zaidi ya Bilioni mbili, tayari shilingi Milioni 147 zimeshatolewa kwa wajasirimali.
Aliyaeleza hayo wakati akitoa taarifa fupi ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, katika program ya Mkono kwa mkono iliyoandaliwa na Idara ya Habari Maelezo na kufanyika Kisiwani Pemba.
Aidha alisema katika mkutano wa UWT, ZEEA ilikabidhi hundi ya shilingi Milioni 75,000,000 kwa vikundi 11 vya wanufaika 67, wanawake 60 na vijana wakiume saba.
Mratib huyo wa ZEEA alisema mfuko huo, umejikita zaidi katika kuwawezesha vijana, akinamama na watu wenye ulemavu, kwa kujenga ukuaji wa uchumi jumuishi.
“Vijana munapaswa kutambua kuwa fedha zipo, munapaswa kufuata utaratibu na kuelea kuwa hizo ni fedha za mikopo, inahitaji uwe na biashara isiopungua miezi sita inayofanya kazi,”alisema.
Alisema kwa sasa wanamfumo ambao utaweza kumsaidia mwananchi kuomba mkopo sehemu yoyote alipo,kwa njia ya mtandao na atajua kila kitu na sio zaidi ya wiki moja.
Aidha mratibu huyo alisema ZEEA itakua na mikopo midogo midogo, ambayo mjasirimali atakua anakopa kupitia simu yake ya Mkononi, ambapo makampuni mbali mbali ya simu yatasaidia katika zoezi la ukopeshaji kidigitali.
Alisema katika mkoa wa kusini Pemba ZEEA inategemea kuanzisha fursa ukarabati wa kituo cha kutolea huduma kwa ajili ya wajasirimali, kwani kituo hicho kitaenda kuboresha uzalishaji wa biadhaa mbali mbali hususan eneo la mwani.
Alisema ZEEA inakusudia kutoa bidhaa iliobora na inayoweza kuuzwa sehemu yoyote duniani, kutokana na ubora wake wa bidha hiyo.
Akijibu baadhi ya maswali ya wajasirimali, mratib huyo alisema ZEEA inashirikiana na PBZ Banka kwa mikopo ya Khalifa Fund, TCB Bank kwa mikopo ya 4.4.2 na CRDB kwa mikopo ya Inuka.
MWISHO