Tuesday, April 13

27 wamefariki dunia 38 wamejeruhiwa kufuatia ajali 63 zilizotokea katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, Januari 2019 hadi Disemba 2020

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

 

WATU 27 wamefariki dunia na wengine 38 wamejeruhiwa kufuatia ajali 63 zilizotokea katika Mkoa wa Kaskazini Pemba kuanzia Januari mwaka 2019 hadi Disemba 2020.

Mwaka 2020 zilitokea ajali 30, walifariki 13 na kujeruhiwa 18 ambapo mwaka 2019 zilitokea ajali 33 , majeruhi 20 na waliofariki ni 14.

Akizungumza na mwandishi wa habari huko Ofisini kwake Wete, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis alieleza kuwa, mwaka 2020 ajali zimepungua ukilinganisha na mwaka 2019.

“Katika mwaka 2020 ajali zilipungua kidogo kutokana na kuwa tunaendelea kutoa elimu kwa madereva na wananchi katika Wilaya zote mbili, ili kudhibiti wimbi la ajali na vifo vitokanavyo na ajali”, alisema Kamanda huyo.

Mapema Kamanda Sadi alifahamisha kwa mwaka 2021 Jeshi la Polisi limejipanga vizuri ili kuhakikisha ajali za barabarani zinaoungua.

Alieleza kuwa kitengo cha Usalama Barabarani (TRO) Mkoa, kimekuwa kikifanya zoezi maalumu kwa madereva kwa kutumia chombo maalumu cha kupimia mwendo pamoja na madereva wote ambao wanalewa huku wakiwa wanaendesha gari.

“Juhudi kubwa ambazo zinachukuliwa Jeshi la Polisi, ili kuhakikisha ajali zinapungua ni kufanya zoezi mara kwa mara barabarani la kuwakamata madereva wote wazembe ambao wanaendesha vyombo kwa kasi au wengine wanalewa na huku wanaendesha gari,” alifahamisha Kamanda Sadi.

“Lakini pia katika matukio hayo ajali nyingi huwa zinasababishwa na waendesha boda boda licha ya kuwa bado hakujawa na sheria rasmi ya bodaboda, lakini inavyoonekana wamepewa ruhusa ya kufanya shughuli hiyo ya kuchukua abiria,” alieleza Kamanda Sadi.

Hata hivyo Kamanda Sadi aliwataka madereva kufuata taratibu na sheria zote za barabara licha ya kuwa barabara hizo ni za zamani lakini zimefanyiwa matengenezo makubwa.

“Kitu cha msingi ninawasisitiza madereva wote kufuata sheria za barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima”, alielekeza.

Aidha amewataka wananchi kuwa makini wanapotembea barabarani, ili kujikinga na ajali.