Monday, June 21

DPP watakiwa kukamilisha upelelezi na kutoa Hukumu ya Kesi zinazowakabili viongozi wa kundi la kiislam Uamsho

Na Thabit Madai, Zanzibar
KATIBU wa Mufti Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume ameiomba ofisi ya Mashtaka (DPP) kukamilisha upelelezi na kutoa Hukumu ya Kesi zinazowakabili viongozi wa kundi la kiislam Uamsho.
Aidha amesema ikiwa kama wataonekana wana hatia muda umefika wa kuweza kuhukumiwa na wakafahamu makosa yao lakini pia kama wataonekana hawana hatia mamlaka itumie busara kuwatoa na kuendelea na maisha ya kawaida.
Kauli hiyo ameitoa leo Ikulu Zanzibar mara baada ya Mkutano maalumu wa Viongozi wa Dini mbalimbali na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Sheikh Khalid alisema hali ya Amani na usalama Zanzibar kwa sasa imeimarika kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi hivyo kuna haja ya Mamlaka husika ikiwemo ofisi ya Mashtaka kukamilisha kesi ya Mashekhe hao na kutoa hukumu kwa kesi zinazowakabili.
“Kutokana na Mazingira ambayo ninayaona hivi sasa Nchi yetu ina Amani na utulivu wa kutosha pamoja na jitihada mbalimbali ambazo amekuwa akizichukua Mhe, Rais wetu kwa kulinda Amani na utulivu wa Nchi hivyo  ushauri wangu kwa ninachokiona kuwa  Mamlaka  iweze kutoa hukumu kwa kesi zinazowakabili viongozi wa Dini ya Kiislamu,”alisema.
Katika maelezo yake alieleza kuwa, hatua mbalimbali za maendeleo zinaonekana zinafanywa na viongozi wa Serikali  sambamba na wananchi kuwa Imani ya Serikali yao hivyo Mamlaka husika zinatakiwa kuanza upya kuangalia kesi zinazowakabili viongozi hao wa dini na kuchukuliwa hatua stahiki.
“Ni muda mrefu umepita toka mashekhe hao kushikiriwa hivyo mamlaka ianze upya kuangalia kwa makini ili kama wanakosa wahukumiwe na kama ikibainika hawana makosa busara itendeke na waendelee na maisha pamoja na kunufaika na Umoja, Amani na  Mshikamani uliopo hivi katika jamii,” aliongeza.
 Aidha Sheikh Khalid alieleza kuwa, hali ya Usalama, Amani na Umoja wa Nchi kwa hivi sasa ipo katika hali nzuri kutokana juhudi za Viongozi wa Serikali kuwaunganisha wananchi pamoja kwa kuhubiri Amani kila kukicha.
“Ukweli kuwa hali yetu ipo vizuri sana viongozi kila siku wanatuhubiria Amani na Umoja wetu hapo nyuma hali haikuwa hivi ndugu zangu waandishi wa habari hata nyinyi mashahidi wananchi sasa Zanzibar wanapendana bila ya kujali tofauti zao za Dini wala siasa,” alifahamisha.
Katika hatua nyingine alimpongeza Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuongoza Nchi kwa uwadilifu huku akizingatia msingi ya haki na usawa.
Hata hivyo Sheikh Khalid alisema kuwa lengo la kumuomba Rais kuonana nae ni kumshauri kwa baadhi ya mambo pamoja na kumpongeza kwa juhudi mbalimbali anazozichukua za kuleta maendelo ya Nchi.
Nae Katibu wa Viongozi wa Dini mbalimbali Askofu Dickson Kaganga alisema Uongozi wa Dk.Hussein Ali Mwinyi umeleta faraja kubwa visiwani Zanzibar kutokana kuwa amewaunganisha watu bila ya kujali tofauti zao za Dini na Siasa.
“Sisi kama viongozi wa Dini tunaunga mkono jitihada zote za Dk Mwinyi ambapo uongozi wake umeleta faraja kwa kuwaunganisha watu bila ya kujali Dini zao hapo nyuma hali haikuwa hivi kulikuwa na mpasuko mkubwa katika jami yetu,” alisema
Alifafanua kuwa jamii hapo awali walikuwa wanaishi kwa migawinyiko kutokana na imani zao za Dini na vyama vyao vya siasa ila uongozi wa Dk. Mwinyi umejitahidi katika kuliondoa hilo na wananchi wanaishi kwa amani na utulivu bila ya kuwepo kwa migawanyiko.
Hata hivyo alitoa wito kwa waumini wa Dini zote kumuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Rais Mwinyi katika kuleta maendeleo ya Nchi.
“Sambamba na hayo ukweli kuwa Rais Mwinyi ni kiongozi msikivu sana tumekutana nae ametusikiliza mashauri yetu hivyo wananchi nawaomba kuendelea kumuunga mkono katika utendaji wake,”
Kwa upande wake Damas Mfoi alisema kuwa Uongozi wa Dini hadi sasa umekuwa unafanya vizuri katika kuwaunganisha watu bila ya kujali itikadi zao hivyo viongozi wa Dini wataendelea kumunga mkono kuhakikisha Zanzibar inakuwa na Amani.
“Tumeshuhudia toka kipindi cha uchaguzi kuwa Rais Mwinyi akikisitiza Amani na utulivu wa Nchi hadi sasa amekuwa rais hivyo sisi kama viongozi wa Dini hatuna budi kuumunga mkono kuhakikisha Zanzibar inakuwa na Amani,” alisema.