Saturday, November 28

JKU wajipanga kulima zaidi.

 

KIASI cha ekari 100 zinatarajiwa kulimwa vilimo mbali mbali na  Jeshi la Kujenga Uchumi Kisiwani Pemba kwa msimu huu wa kilimo 2020/2021.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi huko Ofisini kwake Wawi Chake Chake, MKUU wa zoni Jku Pemba Kanali Machano Kombo Khamis, alisema kwa sasa matayarisho ya kilimo hicho yanaendelea.

Alifahamisha kuwa kwa upande wa kilimo cha mpunga wamepanga kulima ekari 40, muhogo ekari 20, mboga mboga ekari 20,kunde ekari 20, mtama ekari 5 pamoja na mahindi ekari 5.

“Katika msimu huu wa kilimo Jku Pemba tumedhamiria kulima ekari 100 za mazao mchanganyiko ikiwa ni pamoja na mpunga, muhogo, mbogamboga, mtama na mahindi katika makambi yetu,” alieleza Kanali Machano.

Sambamba na hayo Kanali Machano alibainisha kuwa mbali na kilimo lakini pia wanatarajia kuanzisha ufugaji wa kuku wa mayai, nyama, kuku machotara wapatao 4000.

“Lakini pia kila kikosi/kambi tuna mpango wa kufuga kuku wa kienyeji wapatao 500 ambapo matayarisho hayo yameanza kwa kambi ya Jku Chokocho,” alisema Kanal Machano.

“Mbali na hayo pia tunataka kuendeleza mradi wetu wa ufugaji wa samaki katika kituo cha Jku Mwambe, kwa kuingiza vifaranga visivyopungua 5000 katika mabwawa yetu, ambapo hadi sasa tumeshaingiza vifaranga 500 na tumeahaweka ‘oda’ ya vifaranga 1500,” alifahamisha Kanali Machano.

Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo, Kanal Machano alieleza kwa ni mabadiliko ya tabianchi kwani hivi sasa maeneo mengi ya mashamba yao yameingia maji ya mvua na hivyo kufanya trekta lisiweze kufanya kazi vizuri.

“Vile vile kwa upande wa mboga mboga mara nyingi tunakumbana na tatizo la mbegu zisizo bora na hivyo mavuno hayawi mazuri, kwa mfano; mara hii tumepanda matikiti katika shamba letu la Jku Msaani lakini kwa vile mbegu ambazo tuliweza kutumia pale mavuno hayakuwa mazuri,” alisema Kanal Machano.

Sambamba na hayo Kanal Machano alifahamisha kuwa tatizo jengine ni uhaba wa vitendea kazi hasa trekta kwani trekta lililopo ni moja tu kwa Pemba mzima.

Ama kwa upande wa sekta ya ufugaji hasa kwa samaki changamoto kubwa ni ukosefu wa mbegu bora za vifaranga wanaofuga hawako vizuri na hivyo huwasababishia hasara kubwa.

Mapema Kanal Machano aliwataka maafisa na Wapiganaji wa Jku Pemba kurudi katika majukumu yao ya msingi ya uzalishaji ili kujenga uchumi wa Zanzibar kwani uchaguzi umeisha.

Alisema kuwa lengo kuu la Jku ni kuzalisha mali, hivyo aliwasisitiza kushirikiana kwa pamoja ili kuuakikisha malengo waliyopangiwa wanayatimiza bila ya kusimamiwa.

Aidha Kanal Machano aliwataka mabwana shamba na mabibi shamba wa Jku Pemba kuwa na tabia ya kuweka kumbukumbu vizuri kwa kila kinachozalishwa.