Tuesday, May 18

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar azindua Chama cha Madaktari Bingwa wa Maradhi ya Saratani Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema wakati umefika sasa wa kuongezwa kwa huduma za Matibabu katika kutibu  maradhi ya Saratani kwa kuanzisha vituo vipya ili huduma hizo ziwafikie kwa ukaribu Wananchi mahali popote walipo.

Alisema ongezeko hilo muhimu la Tiba ya Saratani italazimika kuzingatia zaidi upatikanaji wa Rasilmali Watu ambao ni Wataalamu mabingwa watakaokuwa makini katika kutoa huduma za Tiba ya Maradhi hayo yanayoonekana kuleta athari Nchini Tanzania.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati akikizindua Rasmi Chama cha Madaktari Bingwa wa Maradhi ya Saratani Tanzania {Tanzania Oncology Socierty – TOS} katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Verde Mtoni pembezoni mwa Jiji la Zanzibar.

Alisema Saratani ni moja ya magonjwa hatari yasiyoambukiza Duniani ambapo zaidi ya Watu Takriban  Milioni 7.9 hufariki Dunia kila Mwaka  Duniani ikiwa ni sawa na asilimia 21% ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambikza Duniani ambapo theluthi mbili wa wagonjwa wa Saratani  wanatoka Nchi zinazoendelea.

Mheshimiwa Hemed alisema Nchini Tanzania kwa vile Saratani inashika nafasi ya Tano kwa Wanaume na  Pili kwa Wanawake  kwa kusababisha madhara ya vifo, Serikali imeamua kuweka muongozo  na Utekelezaji wa  Dira ya Kudhibiti Saratani Nchini ukielekeza kupanua huduma za matibabu ya maradhi hayo.

Kupitia Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanaznia na ya Mapinduzi ya Zanzibar amewapongeza Wataalamu wanaosimamia mapambano dhidi ya Saratani kwa kuanzisha Umoja wao unaolenga kuboresha upatikanaji sahihi wa Tiba ya Maradhi hayo.

Mheshimia Hemed alieleza kwamba Serikali zote mbili zinathamini mchango wa Wataalamu  wa Afya  Nchini katika kusaidia  huduma za Afya na zitaendelea kuimarisha mazingira yao ya Kazi ili waendelee kutoa huduma  bora zitakazosaidia kupunguza vifo  sambamba na kuongeza ubora wa maisha kwa Wagonjwa wa Saratani.

“ Sina shaka yoyote mmeunda chama hichi  kwa lengo la kujiongezea utaalamu zaidi kupitia mafunzo mbali mbali mtakayoandaa ili hatimae muweze kuwahudumia wagonjwa wa saratani vizuri zaidi”. Alisisitiza Mh. Hemed.

Alisema uamuzi wao huo wa kuanzisha Chama hicho umezitia moyo Serikali zote mbili Nchini ukionyesha wazi jinsi walivyojipanga  kupambana na Saratani Nchini mipango ambayo bila shaka Serikali Kuu itahakikisha eneo hilo la Tiba linafanikiwa katika utoaji wa huduma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Madaktari Bingwa ambao bado hawajajiunga na Chama cha Madaktari Bingwa wa Maradhi ya Saratani Tnzania wafanye hivyo ili kupata faida kadhaa kutoka katika Taasisi hio ya Kitaaluma

Mh. Hemed alieleza kwamba mjumuiko mkubwa wa Wataalamu wa Tiba una nguvu na uwezo mkubwa wa kukabiliana na mbadiliko yoyote ya Maradhi pale yanapotokea jambo ambalo pia husaidia kupunguza gharama kwa Wagonjwa wanaolazimika kupelekwa nje ya Nchi kwa matibabu zaidi.

Akitoa Taarifa ya Chama hicho Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Saratani Tanzania {TOS} Dr. Jerry Ndumbalo alisema  Taasisi hiyo ya Wataalamu wa Afya imeanza mchakato karibu Miaka Miwili iliyopita kwa kukusanya Madaktari Bingwa wa fani zote waliofanikiwa kuandaa muongozo wa Taasisi hiyo.

Dr. Ndumbalo alisema Chama hicho kimefanikiwa kupata usajili  rasmi kupitia Sheria Nambari Mia 307 ya Vyama vya Kijamii ya Mwaka 2020 mnamo Tarehe 11 Disemba 29020 kikiwa hakina mipango mipya zaidi ya kuisaidia Serikali katika kuona huduma  za Tiba dhidi ya Saratani zinaimarika Nchini.

Alisema katika kuimarisha upatikanaji wa huduma Bora Nchini za Tiba ya Maradhi ya Saratani Uongozi wa Chama hicho kwa Mwaka 2021/2022 umejipangia kuanzisha Kongamano la Wataalamu wa Maradhi ya Saratani litakalokuwa likifanyika ifikapo Oktoba ya kila Mwaka kwa kufanya tathmini ya faida na changamoto wanazopambana nazo.

Mwenyekiti huyo wa Chama cha Madaktari Bingwa wa tiba ya Maradhi ya Saratani Tanzania alibainisha kwamba kongamano hilo litakwenda sambamba na Kampeni Maalum zitakazoshirikisha Mikoa mbali mbali Nchini ili kuibua Wagonjwa Wapya kabla hawajaathirika zaidi na maradhi hayo.

Alisema Watafiti wa maradhi yasiyoambukiza wamebaini kwamba Hospitali nyingi za Wilaya, Mikoa na Kanda zimekuwa na ucheleweshaji wa Wagonjwa wa Saratani kuwapatia rufaa ya kwenda kupeta Tiba Hospitali kubwa kutokana na uelewa mdogo waliokuwa nao  Madaktari wa Maradhi hayo kwenye maeneo hayo.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi huo Kaimu Waziri wa Afya, Utawi wa  Jamii, Jinsia na Watoto Mh. Simai Mohamed Said alioa rai kwa Wataalamu hao wa Maradhi ya Saratani kujitahidi kuendeleza mashirikiano waliyonayo na wenzao wa Zanzibar  ili waende sambamba katika mfumo wa pamoja.

Mheshimiwa Simai ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar alisema wapo Wagonjwa wengi  wa Maradhi ya Saratani Visiwani Zanzibar ambao kupitia Taasisi hiyo ya Tiba wanaweza kupata afueni ya Matibabu ya Maradhi ya Saratani.

Aliwataka Wataalamu hao wa kutibu Maradhi ya Saratani Nchini wajipange  vyema kwa kuwa na Utaalamu wa ziada kadri maradhi mapya yanavyoibuka ili Taasisi yao ifikie kuwa na uwezo na hadhi ya kutoa huduma Bora Kimataifa mahali popote Ulimwenguni.

 

 

 

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar