Wednesday, January 20

Mjumbe wa Kamat Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mh. Hemed Suleiman Abdulla zungumza na Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Kiwani

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiwaeleza Wananchi juu ya Mikakati ya Serikali Kuu inayopaswa kurejeshewa Heshima yake ya kuwatumikia Wananchi.

Mjumbe wa Kamat Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema Viongozi Wakuu watalazimika kuchukuwa maamuzi magumu katika kuona nidhamu ya Serikali katika kutoa Huduma kwa Wananchi inarejea katika uhalisia wake.

Alisema wakati Serikali inaendelea kupanga safu ya Utendaji katika uwajibikaji wake baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu Wananchi wanapaswa kuunga mkono jitihada hizo ili yale matarajio yao yaweze kufikiwa kwa ufanisi na uharaka uliokusudiwa.

Mh. Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Kiwani  katika Mkutano Maalum ulioandaliwa wa kumpongeza kwa Kuteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi kushika wadhifa huo.

Alisema Chama cha Mapinduzi mbali ya Ilani yake iliyoitangaza kwa Wananchi ambao wameamua kuipa ridhaa ya kuongoza Dola lakini pia kimekusudia kuendelea kuzisimamia Serikali zote mbili ili utekelezaji wa Ilani hiyo ulete mafanikio ndani ya kipindi kifupi kijacho.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Wananchi wanapaswa kushirikiana na Serikali katika kuwafichua wabadhirifu wote waliokula na kujilimbikizia Mali za Umma kinyume na utaratibu wa Serikali.

Alisema Baraza la Mawaziri lililoundwa hivi karibuni tayari limeshaonyesha muelekeo wa kuchapa kazi katika kuwahudumia Wananchi na hilo limeshuhudiwa na Wananchi ambapo baadhi yao muda mfupi baada ya kuapishwa walianza kutoa cheche mara moja.

Mhe. Hemed Suleiman aliwaonya wale wenye tabia ya udokozi pamoja na kuijaribu Serikali kwa kuharibu miundombinu iliyowekwa ikiwemo ya Bara bara kwa kuchomamoto matairi ya gari waelewe kwamba wakati wao wa kufanya vitendo hivyo kwa sasa umekwisha.

“ Ole wao wale Watu wenye utashi wa kuzitumia hasira zao kwa kuchoma moto mipira ya gari na kuziharibu bara bara”. Alionya Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla.

Aliwaasa Viongozi wa Majimbo waliobeba dhima ya kuwatumikika Wananchi lazima wafanye Kazi kwa jitihada katika kutekeleza wajibu wao waliouomba kwa Wananchi wao.

Alisema wapo baadhi ya Waheshimiwa huamua kuyakimbia Majimbo yao na badala yake kutafuta Makaazi mengine jambo ambalo halikubaliki kabisa na linafaa kupigwa vita.

Mapema akisoma Risala ya Wananchi wa Jimbo la Kiwani Mmoja wa Viongozi wa Jimbo hilo Nd. Hassan Hakim alisema kuteuliwa kwake Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kwa nafasi aliyopewa kunatokana na uchapakazi wake uliobeba Uzalendo Mkubwa.

Nd. Hassan Hakim alisema Mkoa wa Kusini Pemba umepata mafanikio makubwa Kimaendeleo kutokana na usimamizi mzuri wa Mh. Hemed wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Mkoani na baadae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba.

Wananchi hao wa Jimbo la Kiwani kupitia Mkutano huo wamempongeza Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein kwa usimamizi mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM iliyofikia zaidi ya asilimia 98% katika Utekelezaji wake ndani ya Miaka Mitano ya Pili ya Utawala wake kuanzia Mwaka 2015/2020.

Baadhi ya Wananchi waliohudhuria Mkutano wa kumpongeza Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla uliofanyika hapo Uwanja wa Michezo wa Kijiji cha Kiwani Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.

 

 

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar