Tuesday, January 19

MTOTO mmoja mchanga amekutikana ndani ya sinki la choo cha hospitali ya Chake chake Pemba

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MTOTO mmoja mchanga, anaekisiwa kuzaliwa kwa miezi saba, amekutikana ameshafariki dunia, ndani ya sinki la choo cha hospitali ya Chake chake Pemba, huku mama aliyemzaa mtoto huyo, akiwa anatafutwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kusini Pemba.

Mwandishi wetu ambae alifika hospitali ya Chake chake, alimshuhudia mtoto huyo akiwa ndani ya sinki hilo, kwenye choo kinachotumiwa na wagonjwa wanawake, wanaofika hospitalini hapo.

Akizungumza na mwanadishi wa habari hizi, kwenye eneo la tukio, Daktari dhamana wa hospitali ya Chake Chake Ali Omar Khalifa, alisema mtoto huyo, aligundulika majira ya saa 3:00 asubuhi.

Alisema tukio hilo, linaonekana kufanyika baina ya saa 1:00 asubuhi ya Januari 9 mwaka huu, wakati mmoja wa wagonjwa waliofika hospitalini alipokwenda chooni kujiasaidia.

Alisema baada ya hapo, mtu huyo alitoa taarifa kwa wafanyakazi wa hospitali, na baada ya kugundulika alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na watendaji wa Idara ya Ustawi wa Jamii.

Alisema, mtoto huyo anaonesha kuzaliwa kwa miezi saba, ambae ni wa kike na baada ya kuondolewa hapo, alionekana akiwa na zalia lake na tayari ameshafariki dunia.

Daktari huyo Dhamana alisema, taarifa za awali inasemekana kuwa, majira ya saa 12: 55 asubuhi ya Jumamosi, daktari wa zamu aliwapokea watu wanne, akiwemo mwanamke mmoja.

Alifafanua kuwa, watu hao walikuwa wamemshikilia mwanamke huyo kama mgonjwa mahatuti na kumpeleka kwa daktari wa zamu, na kisha kuomba ruhusa ya kwenda kujisaidia.

“Baada ya kwenda chooni kujisaidia, kisha hawakutokea tena hospitali hapo na kuondoka na buku lao, kabla ya kuchukuliwa taarifa na kisha daktari huyo wa zamu, kupokea wagonjwa wengine,’’ alieleza.

Alisema majira ya saa mbili baadae, ndipo walipoarifiwa na mmoja wa wagonjwa waliokwenda chooni huko kujisaidia, na kisha kumshuhudia mtoto huyo mchanga akiwa ameshafariki.

Mkuu wa wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, alisema wamelipokea tukio hilo kwa mshituko mkubwa, na kusema lazima Jeshi la Polisi lifanye haraka, kumtafuta aliyefanya tukio hilo.

Alisema, huo ni aina ya uhalifu ambao haukbaliki ndani ya jamii, jambo ambalo limeitia dona wilaya, hasa ikiwa katika mpango wa kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Wanawake na wanaume ambao husababisha kupatikana kwa mimba, lazima mimba hiyo wailee kwa pamoja, ili kuhakikisha mama husika anajifungua katika mazingira salama,’’alisema.

Kwa upande wake Afisa wa Ustawi wa Jamii, Hifadhi ya Mtoto wilaya ya Chake chake Rashid Said Nassor, alisema walipokea taarifa ya kukutikana mtoto mchanga akiwa ameshafiriki dunia majira ya saa 3:45 asubuhi.

Alisema, baada ya kupokea taarifa hiyo, walifika eneo la tukio na kisha kuwasiliana na Jeshi la Polisi na baada ya yao kufika, waliratibu shughuli za maziko katika shehia ya Kichungwani, kabla ya mtoto huyo kuchukuliwa sampuli yake ya damu.

Alisema tukio hilo, limewatia simanzi kubwa hasa kwa vile wamekuwa wakitoa elimu kila siku ya hifadhi na matunzo ya mtoto, kuanzia akiwa tumboni hadi kufikia umri miaka 18.

“Ni kweli, kuna mtu asiejulikana amekwenda kujifungua ndani ya choo cha hospitali ya Chake Chake na mtoto kufariki dunia, na sasa ameshakamilishiwa taratibu za mazishi mtoto huyo,’’alieleza.

Hata hivyo Afisa huyo, amelisisitiza Jeshi la Polisi, kumtafuta mama aliyefanya hivyo, ili akamatwe na kisha kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Daktari wa zamu katika hospitali ya Chake Chake, Hamir Juma Suleiman aliyewapokea mwanamke mmoja na wanaume watatu anayetuhumiwa kuwa ndie aliyemzaa na kisha kumtupa mtoto huyo, alisema walifika na kisha kukabidhi buku lao kwake.

“Walipokwishafika na baada ya kunikabidhi buku lao, kisha waliomba kwenda chooni, lakini hawakurudi tena, na alikuja mmoja wao kuchukua buku na kuondoka,’’alieleza.

Kwa mwaka jana pekee, watoto wawili wachanga waliokotwa wakiwa hai baada ya kutupwa, ingawa kwa mtoto kuonekana akiwa ameshafariki dunia, hili ni tukio la kwanza katika kipindi cha miaka mitatu.