Wednesday, January 20

Tuhuma za kutorosha na kubaka bado zamsotesha rumande.

 

Mtuhumiwa Bakar Mbwana Juma mwenye umri wa miaka 32 mkaazi wa Jomvu Kengeja anaekabiliwa na shitaka la Kumtorosha na Kumbaka msichana mwenye umri wa 17 ameiambia mahakama ya Mkoa Chake Chake kuwa yeye hahusiki na tukio hilo kwani muda uliotajwa kutenda kosa hilo alikua kwenye kibanda akinywa kahawa.

Aliambia mahakama hiyo kuwa yeye ni mfanya kazi wa ujenzi wa nyumba hivyo anakawaida ya kurudi kazini  baina ya saa moja hadi saa moja na nusu za usiku na mara zote hufikia kwenye mkahawa kabla ya kwenda anakoishi.

Alidai kuwa siku ambayo alituhumiwa kufanya tukio hilo alirudi kazini majira ya moja za usiku na kifikia mgahawani na kupata kahawa akiwa yeye na marafiki zake.

Alifahamisha kuwa baada ya kunywa kahawa alirudi nyumbani na kuigia chooni kwa ajili kujiandaa na sala ya Isha na kisha kwenda msikitini.

‘’Nashangaa sana  wakati huo wa saa mbili nitatorosha saa ngapi na nitabaka saa ngapi hilo haliwezekani’’ Alidai mtuhumiwa huyo.

Alidai kuwa kabla ya kutokea kwa tukio  hilo walikuwa na ugomvi kati yake na kaka wa anaedaiwa kumfanyia  udhalilishaji.

Wakili wa mtuhumiwa huyo Abeid  Mussa ameiomba mahakama hiyo kulipangia siku nyengine shauri hilo kwa vile bado yuko shahidi mwengine wa utetezi.

‘’Mheshimiwa naomba ighairishe na uipange siku nyengine kwa ajili ua kusikiliza shahidi mwengine’’ Alidaiwakili .

Baada ya mtuhumiwa huyo kupanda kizimbani akisubiri taratibu za Mahakama ndipo mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka DPP Juma Ali Juma alidai kuwa shauri hili lipo kwa ajili ya utetezi.

‘’Mheshimiwa hakimu shauri hili lipo kwa ajili ya ushahidi na kwa upande wetu hatunashaka na hilo’’, alidai mwendesha mashtaka huyo.

Hakimu wa mahkama hiyo Lusiano Makoe Nyengo alikubaliana na upande wa mashtaka na kumtaka mtuhumiwa huyo ajitetee.

Ilidaiwa mahakamani hapo mtuhumiwa huyo kosa la kwanza alitenda tarehe 2/6/2020 bila ya halali na bila ya ridhaa ya wazazi wake alimtorosha msichana wa miaka 17 kutoka nyumbani kwao na kumpeleka nyumbani  anakoishi .

Kufanya hivyo ni kosa  kinyume na kifungu  cha 113[1] [a] cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar .

Kosa la pili  alitenda siku hiyo hiyo majira ya sa 2; 00 za usiku katika kijiji cha Kengeja wilaya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.

Ilidaiwa kuwa bila ya halali na bila ya ridhaa ya wazazi wake alimbaka msichana huyo wa miaka 17 ambapo kufanya hivyo ni kosa kisheria kifungu cha 108[1] [2] [e] na 109 [1] sheria ya adhabu sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Shauri hilo litasikilizwa tena mahakamani hapo tarehe 12/10/2020 kwa ajili ya kusikilizwa shahidi mwengine.