Sunday, August 1

VIDEO: Wazazi na Walezi wametakiwa kuwalinda watoto wao juu ya vitendo vya udhalilishaji hasa katika kipindi hiki cha sikukuu .

NA KHADIJA KOMBO-PEMBA

Wazazi na Walenzi nchini wametakiwa kuwa makini katika kuwalinda watoto wao juu ya vitendo vya udhalilishaji hasa katika kipindi hiki  cha sikukuu ambapo vitendo hivyo hushamiri zaidi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa  TAMWA Zanzibar Dk Mzuri Issa katika taarifa yake aliyo itoa juu ya tahadhari ya kuwalinda watoto na vitendo vya udhalilishaji katika kipindi hiki cha sikukuu ya Eid EL HAJJ.

Amesema Zanzibar kama sehemu nyengine za dunia watoto husheherekea sikukuu kwa kwenda maeneo mbalimbali ya sherehe hizo hivyo watu wenye nia ovu hutumia mwanya huo kwa kuwadhalilisha watoto kijinsia.

Amesema sikukuu ni siku ya furaha hasa kwa watoto lakini wazazi hawana budi kuchukua tahadhari katika kuwalinda watoto wao ili wasije wakaharibu furaha zao.

Amewataka wazazi na walezi kufahamu kuwa watu wenye nia ovu wana ishi karibu na jamii hivyo ni rahisi kuwaona watoto na kuwahadaa kwa kuwarubuni kwa kuwapa mkono wa idi na hatimae kufanya unyama huo.

Hivyo amewataka wazazi kutokuwacha watoto kutembea katika viwanja vya sikukuu peke yao pamoja na kuwavalisha nguo zisizo kwenda na maadili ya ki Zanzibar  ili kuepuka maafa hayo.

Sambamba na hayo ameliomba Jeshi la Polisi nchini kuongeza kasi ya ulinzi ikiwemo barabarani ili kuepusha ajali za watoto zinazoweza kuepukika.

Wakati Zanzibar na  Tanzania kwa ujumla zinaungana na mataifa mengine kushereheka sikukuu hii ya Eid El Hajj   Afisa kutoka Ofisi ya Mtakwimu mkuu Rahma Hassan amesema vitendo vya udhalilishaji vimeongezeka  kutoka kesi  66 katika mwezi wa May ambapo mwezi wa June ziliripotiwa kesi  97 .

Katika matukio hayo  97 ya mwezi wa June,  49 ni kesi za kubaka ,11 kulawiti , 21  kuingiliwa kinyume na maumbile, 10 kutorosha na 7 shambulio la aibu.

Akifafanua kuhusu mwezi wa Mei mwaka huu amesema matukio yote yalikuwa ni 66  ambapo kesi za kubaka zilikuwa ni 43,kulawiti 7,kutorosha 7, nashambulio la aibu 9.

KUANGALIA VIDEO BOFYA HAPO CHINI