Tuesday, April 13

VILABU vya Pemba vyamwaga mboga.

VILABU vinavyoshiriki ligi daraja la kwanza Taifa Kanda ya Pemba, zimesema kuwa hawezi kucheza mpira kama rais wa shirikisho la soka Zanzibar (ZFF) Seif Kombo Pandu, hatoondoka madarakani pamoja na watendaji wake wote.

Vilabu hivyo vimesema pia hawana imani na bodi ya ligi, hivyo viongozi wa bodi hiyo wanapaswa kukaa pembeni ili kupisha mpira wa Zanzibar uchezwe.

Kauli hizo zimetolewa na wadau wampira wa miguu Kisiwani Pemba, wakati wakikao na viongozi wa Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, wakiongozwa na waziri wawizara hiyo Tabia Maulid Mwita, katibu Fatma Hamad Rajaba na Naibu Katibu Khamis Abdalla Said, kikao kilichofanyika Gombani mjini chake Chake.

Ali Seif Said Rais wa Timu ya Mwenge alisema iwapo viongozi hao watakaa pembeni basi wao watakuwa tayari kucheza ligi muda wowote na ratiba kuipanga wenyewe.

Alisema kuwepo kwa Seif kombo madarakani na kutokukubali ushauri anaopatiwa na kuiongoza ZFF kifalme, umepelekea soka la Zanzibar kuyumba na huku vilabu vya Pemba vikisubiri kushushwa madaraja matatu.

“Kama huyu Rais hatoondoka madarakani na sisi tutaendelea kutokukubali kucheza ligi, yote haya yanayotokea yeye ndio chanzo kikubwa kwa katika mpira wa zanzibar”alisema.

Msemaji wa Timu ya Younger Islander Mohamed Khatib, alisema wakati umefika kwa katiba ya ZFF na kanuni zilizopo kufanyiwa marekebisho, kwani haiwezekani viongozi wote wa mpira kutoka upande mmoja.

Alisema mpira unabeba nembo kubwa ya nchi pale vilabu vinapoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa, hivyo hawatocheza mpira iwapo viongozi wa soka wataendelea kusalia madarakani, badala yake wanapaswa kupisha uchuguzi dhidi ya tuhuma mbali mbali zinazotolewa.

Alisema sababu kubwa ya kutokuwa na imani na Kiongozi huyo, kutokana na uwongo, wizi na kutokukubali kushauriwa, hivyo vilabu vya Pemba vimechoka kudhulumiwa na haviko tayari kuendelea kufanywa ngazi na hawakubaliani na mambo yoyote yanayotendeka kwa sasa.

“Kanuni ya mashindano inasema ligi mikondo miwili, ukiendeshwa mkondo mmoja hauwezekani mwisho wa siku waamuzi walitoka unguja na kuchezesha Pemba, jambo ambalo ni kuwadharau wa waamuzi wa Pemba”alisema.

Katibu wa timu ya Umeme Suwedi Hamad alisema mwaka 2019 ligi ilisimama zaidi ya mara mbili na sio sababu ya COVID 19, bali sababu kubwa ni fedha za waamuzi walizokuwa wakidai zaidi ya shilingi Milioni 15, zikijumuisha michezo ya ligi kuu, ligi daraja la kwanza na FA, ambazo hawakulipwa na mpira ukachezwa mzunguruko mmoja.

Alifahamisha jambo la kusikitisha Pemba waliweza kukusanya fedha zaidi ya hizo wakati wausajili na ada mbali mbali za mashindano na kuziingiza katika ACCOUNT ya ZFF Unguja, hivyo vilabu vinataka kujuwa wakikubali kucheza ligi fedha zao watalipwa na kiongozi gani pale ligi itakaposhindwa kuendelea.

Hata hivyo aliomba kurudishwa kwa ofisi ya ZFF Pemba pamoja na Account, ili malipo ya Pemba yabakie pemba na sio kutumiwa vyengine kama utawala uliopita ulivyoendesha ligi kwa kutumia account ya Pemba.

Katibu wa timu ya Chipkizi Ali Juma Khamis, alisema vilabu vinahitaji katiba ya ZFF na Kanuni yake kufanyiwa marekebisho, uwongozi wote uliopo madarakani uweondoke, mgawanyo waligi urudi wa zamani Pemba yao na Unguja yao mwisho wa siku inachezwa nane bora.

Kwa upande wake Mdau Mawalimu Ali Ahmed kutoka Timu ya Mkoroshoni, aliitaka serikali kutambua kuwa vilabu vya Pemba havijagoma kutokucheza mpira, kwani ndio maradhi yao bali hawanaimani na Viongozi wa ZFF waliopo madarakani.

“sisi tutacheza mpira pale tu viongozi wote pamoja na bodi yao kuondoka, kwani wameshindwa kusimamia mpiara wa Zanzibar na kupelekea hapo walipofika sasa”alisema.

Kwa upande wake Mwamuzi Mstaafu mwenye beji ya FIFA Ali Juma Salim, alisema malipo makubwa ya waamuzi ni matusi wanapokuwa uwanjani, aliwashukuru Viongozi wa vilabu kwa kuwasimamia madeni yao, ambapo zaidi ya milioni 15 wanakidai chama hicho.

Alisema tatizo kubwa ni kufanyiwa marekebisho kanuni na katiba ya ZFF, pamoja na kusikitishwa na Viongozi wote wa ZFF kuwepo Unguja.

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Khamis Abdalla Said, alisema wizara ipotayari kuendeleza michezo na Pemba kuhakikisha mpira unachezwa.

Naye katibu Mkuu wa Wizara hiyo Fatma Hamad Rajab, alisema lengo la kikao hicho ni kusikiliza malalamiko ya wadau wa soka, ili kuona jinsi gani wanafanya na ligi inachezwa.

Kwa upande wake waziri wa habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, aliwahakikishia wadau wamichezo mpira unachezwa Pemba, huku akiwataka kuwa kitu kimoja kwa kitendo ambacho kitaamuliwa hivi karibuni.

Alisema serikali ya awamu ya nane sio serikali ya kuchezewa, na hatokuwa tayari kuondoshwa madarakani kwa kisingizio cha mpira pemba hauchezwi kutokana na kuwepo kwa migogo inayosababishwa na mfalme wa ZFF.

Aidha aliwahakikishia wadau hao kuwa account ya ZFF Pemba itarudi, pamoja na kuwepo na ofisi yake na inafanyakazi kama ilivyokuwa miaka ya nyumba.

“Sisi kila siku tunakwenda mbio kutafuta wafadhili wa ligi ya Zanzibar lakini wanakwama kutokana na uongozi uliopo hivi sasa wa magumashi, itafika pahali uongozi utabadilika kutokana na maamuzi ambayo yanakuja tena kwa vitendo”alisema.

Hata hivyo aliwataka wadau hao kuondosha tafauti zao na kuwa kitu kimoja, katika maamuzi yatakayochukuliwa huku akivitaka vilabu kujiandaa kushiriki katika ligi muda wowote.

Akizungumzia suala la amadeni alisema atahakikisha analifanyia kazi, kwani wanampango wakuingiza Mkaguzi wa ndani wa Fedha na kufanya ukaguzi tokea kipindi walichoingia madarakani viongozi waliopo na kujuwa fedha zilivyotumiwa.

Kikao hicho kilitanguliwa na mabango mbali mbali yaliyokuwa na ujumbe wa kumkataa Rais wa shirikisho la soka Zanzibar, pamoja na bodi ya ligi na viongozi waliopo madarakani kwa kuwataka kujiuzulu nyazifa zao