Tuesday, January 19

WAKULIMA wa vanila katika shehia ya Mtambwe Kaskazini Wilaya ya Wete Pemba, wameiomba Serikali kuwatafutia soko la uhakika

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAKULIMA wa vanila katika shehia ya Mtambwe Kaskazini Wilaya ya Wete Pemba, wameiomba Serikali kuwatafutia soko la uhakika, ili kupata fedha zitakazowasaidia kuwakwamua na maisha magumu.
Walisema kuwa, kwa kipindi hiki vanila imekuwa na bei kubwa zaidi ukilinganisha na viungo vyengine, ingawa soko lake ni la kutegemea wageni tu, jambo ambalo wakati mwengine zinakaa muda mrefu bila ya kununuliwa.
Wakizungumza wakati walipotembekewa na uongozi wa Kamisheni ya Utalii Pemba kwa lengo la kuupa hadhi ukulima wa viungo na kuwa wa utalii, wakulima hao walisema kuwa, ipo haja kwa Serikali kuwatafutia soko la uhakika, ili wauze bidhaa yao hiyo kila siku.
Walieleza kuwa, iwapo kutakuwa na soko la uhakika wanaamini kwamba wananchi wa kisiwa cha Pemba watanufaika kiuchumi kutokana na kwamba kilo moja ya vanila sasa ni shilingi 850,000.
“Sio watu wengi wanaolima vanila kutokana na kuwa hakuna soko la uhakika, tunaiomba Serikali itutafutie soko ama wanunue wao kisha wazisafirishe, kwa sababu inahitajika zaidi vanila kutoaka Pemba kutokana na kiwango chake”, walisema wakulima hao.
Mkulima Hamad Omar Mwita alie na shamba lake Uondwe Mtambwe alisema, pia wanahitaji mashine za kuweza kugundua magonjwa yanayoisibu miti hiyo ya vanila.
“Wakati mwengine unakuja kuona vanila zimepukutika (kuanguka) tu, hujui zimesibiwa na nini, lakini tukipata mashine tutaweza kujua na kudhibiti magonjwa mapema”, alisema Mkulima huyo.
Alieleza kuwa, alipata elimu ya kupanda vanila kupitia Jumuiya ya kuhifadhi misitu asili Pemba (CFP) na tayari ameshawafundisha wakulima wapatao 31 ndani na nje ya kisiwani hiki.
Kwa upande wake mkulima Amina Ali Juma alisema, katika kilimo hicho lazima uangalie ardhi kwanza kabla ya kupanda, hivyo wameomba kupatiwa wataalamu, ili kuweza kuimarika zaidi kwa zao hilo, jambo ambalo litasaidia kuzalisha kwa wingi.
“Sisi hutufundisha Hamad Mwita kuchanganya udongo ambao utaifanya ardhi kuwa na virutubisho lakini na wakati mwengine ana pirika zake, hivyo Serikali ituwekee wataamu ambao wakati wowote wanapatikana”, alisema.
Aidha alieleza kuwa, wanahitaji wapate maji (drop irrigation), ili kukuwa na kustawi vizuri zaidi, kwani miti hiyo haitaki kupandwa sehemu yenye maji mengi.
Nae mkulima Hamad Khatib Hamad alisema, licha ya ukulima huo wa vanila, pia wanalima viungo vyengine kama, mdasini, hiliki, pilipili manga na karafuu, kwa lengo la kujikwamua kimaisha.
“Hiki ni kikundi lakini kila mwanakikundi ana shamba lake la viungo, hivyo tunaomba tutatuliwe changamoto zetu ili maisha yetu yaboreke”, alieleza mkulima huyo.
Afisa Utalii Mkoa wa Kusini Pemba, Mohamed Ali Juma alisema, Serikali kupitia ilani yake ya chama mwaka 2025, imeipa ukulima wa viungo kuwa ni sehemu ya utalii, hivyo wanatarajia kwamba changamoto za wakulima hao zitapatiwa ufumbuzi.
“Pamoja na changamoto zinazowakabili lakini msivunjike moyo, endeleeni kulima kwa vile viungo vina bei kubwa hasa vanila, kwani mtapata kutatua shida zenu”, alifahamisha Afisa huyo.
Hivi karibu Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kisiwani Pemba kwa kushirikiana na CFP pamoja na shirika la PDF kutoka Dar-es-Salaam walitoa mafunzo kwa wadau wa taasisi za Serikali na kusema kuwa, jumla ya Euro Milioni 5 zimefadhiliwa na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya wakulima wa viungo Zanzibar.
Kamisheni ya Utalii Pemba ilifanya ziara ya kuwatembelea wakulima wa viungo katika shehia ya Mtambwe Kaskazini, lengo ni kuangalia changamoto zinazowakabili ili kutafuta njia mbadala ya kuzitatua.