Sunday, August 1

Waumini wa dini ya kiislamu watakiwa kuongeza nguvu katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji.

NA KHADIJA KOMBO-PEMBA.

Waumini wa Dini ya Kiislam wametakiwa kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji wa kijinsia ili kuhakikisha nchi yetu inabaki salama.

Wito huo umetolewa na Imamu wa Msikiti wa Masjid Rahman  Chanjaani chake chake Pemba Sheikh Shehe Suleiman Hassan alipokuwa akizungumza na waumini hao mara baada ya sala ya Eid.

Amesema licha ya juhudi kubwa  zinachukuliwa na viongozi pamoja na wanaharakati mbali mbali bado vitendo hivyo vinaendelea kushamiri hivyo  wauumini hao ni vyema  kutafakari  upya namna ya kukabiliana na vitendo hivyo ili kuhakikisha kuvinakomeshwa kabisa  katika jamii zetu.

Amesema tatizo na udhalilishaji si  jambo la kufumbiwa macho kwani ni mambo ambayo yanapoteza ndoto za watoto wengi  katika kupanga misingi imara ya maendeleo yao hapo baadae.

“kama waumini lazima tushirikiane katika kuviibua vitendo hivi  pamoja na kukemea kwa nguvu zetu zote”alisema Sheikh Shehe.

Akizungumzia kuhusu watoto kusherehekea sikukuu ya Eid  hajj amesema siku hii ni siku ya furaha na watoto  na hupata fursa ya  kutembelea katika maeneo mbali mbali  lakini wazazi wanatakiwa kuwa makini  katika matembezi hayo ili kuwanusuru na  majanga  yanayoweza kutokea.

Pia Sheikh Shehe amewaomba madereva kuawa waangalifu wanapokuwa barabani ili kuepuka ajali zisizokuwa na lazima.

Sikukuu ya Eid Hajj  husherehekewa ulimwenguni kote  kwa kuwaunga mkono waislamu waliokwenda  Makka Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hijja   ikiwa ni kutimiza nguzo ya tano ya dini ya Kiislam.