Tuesday, April 13

ZFF yaendelea kukaliwa kooni

 

NA ABDI SULEIMAN.

BADO upepo mbaya unaendelea kulisakama shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), juu ya malipo ya Fedha za timu za mikoa ambazo zilitolewa na shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF), tokea mwaka 2019 hadi sasa hazijulikani zilipo.

Hayo yameelezwa na viongozi wa timu hizo upande wa Kisiwa cha Pemba, ambao walidai kuchangishana na vijana wao pamoja na nyengine kuazima ili kuweza kushiriki mashindano ya Vijana U 17 mwaka juzi Kibaha Mkoa wa Pwani.

Wakizungumza mbele ya Viongozi wa Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, wakiongozwa na waziri wa wizara hiyo Tabia Maulid Mwita, Katibu Mkuu Fatma Hamad Rajab na Naibu Katibu Mkuu Khamis Abdalla Said, wamesema kuwa tayari walishapelekwa mahakamani juu ya fedha hizo ambazo wao mpaka sasa bado hawajazipata.

Kiongozi wa Timu ya Mkoa wa Kusini Pemba Kassim Juma Mussa, alisema gharama zao ni shilingi Milioni 1,740,000/= ambazo walizotumia katika mashindano hayo.

“Sisi tulipofika Kibaha TFF walitwambia kama fedha bado hawajaingiziwa na wakiingiziwa watatutumia wenyewe ili turudishe tulikoazima, chakushangaza TFF walizituma fedha hizo tokea Septemba 12/2019 katika Account ya ZFF lakini sisi Viongozi hazijatufikia hadi sasa”alisema.

Naye Jongo Juma Jongo mkuu wa Msafara kwa timu ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, alisema timu za mikoa zinaposhiriki mashindano hayo, zinatakiwa kujigharamia wenyewe mpaka zinapofika Tanzania bara ndio zinakuwa katika mikono ya TFF.

Alisema gharama zote wanazotumia wakiwa katika safari ikiwemo nauli za mabasi, meli na chakula wanarudishiwa baada ya kufika bara, gharama hiyo hujumuiyshwa kwenda na kurudi kwa timu zilikotoka.

“Kwamujibu wa TFF sisi tulitakiwa tusafirishe vijana 25 na walikwenda Kibaha, kwenda tulitumia Milioni 1,740,000/= fedha hizo tulitakiwa tulipwe mara mbili ili kupata na kurudia kima hicho hicho, chakushangaza mwaka hule ZFF ilililazimisha TFF kuziingiza fedha hizo kwenye account yao, baadae TFF wakatutumia sisi mikoa mgawanyo wa fedha kwa mikoa yote kama ilivyokua lakini hadi sasa hakuna kilichopatikana”alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Msafara wa Timu ya Mkoa wa Kaskazini Pemba Hamad Ali Bakari, alisema tayari alishashtakiwa Polisi kwa madeni ambayo yanaonekana yameshalipwa lakini yeye bado hajazipata mpaka sasa.

Alisema kutokana na hali hiyo amekosa imani na Rais wa shirikisho hilo, pamoja na katibu wake aliyekuwepo madarakani huku akimtaka waziri hiyo kufuatilia madeni hayo ili viongozi hao waweze kurudisha fedha zao walikozikopa.

“Kuondoka Kwao lazima kwanza watulipe fedha za watu mimi mpaka hii leo bado ninakesi ya Polisi juu ya fedha hizo za vijana ambao walikwenda Kibaha”alisema.

Kwamujibu wa barua kutoka TFF, kwenda kwa taibu Mkuu wa ZFF, yenye kichwa cha habari kinachosema “YAH:Nauli ya Mikoa ya Zanzibar mashindano ya U 17 2019”.

Barua hiyo imesema kuwa “Tunapenda kukutaarifu kuwa tulifanya malipo kwenye Account ya ZFF Shilingi 5,651,000/= tarehe 12/9/2019 kwa ajili ya kuwarudishia nauli za mikoa yote ya Zanzibar walipokuja kwenye mashindano ya U 17 yaliyofanyika kibaha mwaka 2019 kama ifuatavyo”.

Kaskazini Unguja TSH 745,000/=,Kaskazini Pemba TSH 1,740,000/=, Kusini Pemba TSH 1,740,000/=,Kusini Unguja TSH 876,000/= na Mjini Magharibi TSH 550,000/=, barua hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mashindano shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Salum S.Madadi.

Kwa upande wake Waziri wa habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, aliahidi kufuatilia madeni hayo kwenye shirikisho la Mpaira wa miguu Zanzibar na kuona yanalipwa kwa wahusika kama iliyotolewa na TFF.

Alisema atahakikisha katika uongozi wake viongozi wa ZFF wanabadilika au wanaondoka madakani, ili mpira wa Zanzibar uweze kuendelea.

Waziri huyo alisema kwa muda mrefu uongozi wa ZFF uliopo madarakani umekuwa na mataatizo mengi, ligi pemba haichezi sababu uongozi, timu za mikoa fedha zao hawajalipwa sababu uongozi wa ZFF, huku akiwataka viongozi hao kuwa na subra katika kipindi kifupi huku wakitarajia mabadiliko makubwa kutoka kwa viongozi wa wizara waliopo sasa.