WAANDISHI watakiwa kutokua chanzo cha migogoro

NA MWANDISHI WETU.

MWANDISHI wa Habari Mwandamizi Pemba na Mkufunzi wa masuala ya habari Said Mohamed Ali, amesema waandishi ni nyenzo muhimu ya kuepusha migogoro na kujenga amani katika nchi, ili kufikia huko wanapaswa kuwa makini katika habari wanazoziandika kutokuwa chanzo cha migogoro ndani ya jamii.

Alisema iwapo waandishi hao watatumia vyema kalamu zao katika habari zao, basi hakutakua na migogoro yoyote inayoweza kutokea, iwapo watacheza na wakati katika kuandika habari zao.

Mkufunzi huyo aliyaeleza hayo wakati wa mafunzo ya siku mbili juu ya umuhimu wa Habari na Amani, mafunzo yaliyofanyika mjini Chake Chake.

“Vyombo vya habari vinaweza kuwa jukwaa la kuchochea utawala bora –  Uwazi, uwajibikaji, utawala wa sheria, migogoro haya yote ni ya msingi sana kama wananchi watapata habari za usawa, sahihi, kwa wakati na zisizochochea migogoro na zinazohimiza maridhiano”alisema.

Alisema habari ni muhimu sana katika kuchochea mabadiliko  chanya ya watu, mahusiano mazuri, maridhiano, kupunguza hamasa mbaya, misimamo  mikali, kuleta maridhiano, mabadiliko ya tabia.

Alieleza mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wa kuripoti habari za migogoro na amani ni pamoja na kutokumuumiza mtu, kuelewa chimbuko, kupaza sauti kwa usawa, kuunga mkono juhudi za maridhiano, kupiga debe uwepo wa sheria, miongozo na matamko yanayoleta maridhiano.

Mapema mwenyekiti wa PPC Bakar Mussa Juma, aliwataka aliwataka waandishi wa habari kuzitumia vyema kalamu zao kwa kuhubiri zai masuala ya amani ndani ya nchi yao, kwani vyombo vya habari ni kiungo muhimu cha kuwaunganisha wananchi na serikali yao.

Alisema kuwa waandishi wa habari ni kiungo muhimu cha kuwaunganisha wananchi, aliwataka kufuata sheria na maadili ya kazi zao jambo ambalo halitopelekea kuwa chanzo cha migogoro.

“Mwandishi wa habari unapotaka kuandika habari yako lazima uwe na taarifa sahihi, kufanya balanzi ya habari yao, kuwa sahihi kujenga utaratibu wa kujitoa kufanya kazi katika jamii, ili kutatua changamoto zilizopo kwa wananchi”alisema.

Akizungumzia Klabu ya waandishi wa habari Pemba, mwenyekiti huyo alisema kwa sasa klabu hiyo imebadilika kwani imekua ikitafuta miradi wenyewe na kuipeleka kwa waandishi wa habari na kuwajengea uwezo.

Kwa upande wao waandishi wa habari Ali Massoud Kombo, alisema waandishi wa habari wanapaswa kufuata utaratibu wa kuzipitia sheria zinazowalinda, ili waweze kufanya kazi kwa kujiamini na bila kuyumbishwa.