PPC waadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari Pemba.

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAANDISHI wa habari kisiwani Pemba, wamekumbushwa kuwa, iwapo wataandika habari bila ya upendeleo, zinakuwa daraja la kufikia maendeleo ya kweli kwa jamii iliyowazunguruka.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu tawala mkoa wa kaskazini Pemba Khatib Juma Mjaja, alipokuwa akizungumza na waandishi hao na wadu wao, kwenye mkutano uliofanyika ukumbi wa Maktaba Chake chake, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari, duniani.

Alisema, habari ni kichecheo muhimu na adhimu katika kuleta maendeleo kwa jamii, kwa kule habari hizo zilizoandikwa kwa uweledi watazitumia.

Alieleza kuwa, moja ya shaka wanayokumbana nayo jamii, ni kukosa habari za aina zote, kwa kule baadhi ya waandishi wa habari, kuegemea habari za aina moja katika kazi zao.

“Mwandishi kama utajikita kuandika habari za aina moja, na nyingine kuziacha huitendei haki jamii yako, habari yako inaweze isiwe kichecheo cha maendeleo,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Katib tawala huyo, aliipongeza Klabu ya waandishi wa habari PPC, na UTPC, kwa kufanya mkutano huo ambao, utatoa nafasi kwa wadau na waandishi kufahamiana zaidi.

Mapema Mwenyekiti wa PPC Bakar Mussa Juma, alisema siku ya uhuru wa vyombo vya habari, ni nafasi kwa waandishi kutathimini kazi zao na iwapo kuna changamoto wanaweza kuzindosha vipi.

Alieleza kuwa,, kwa vile PPC iliamua kuwaalika na wadau ‘sources’ itakuwa ni nafasi kwao kuwakosoa na kuwapongeza waandishi hao wahabari, namna wanavyofanyakazi zao.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa PPC, aliwataka wadau hao kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari, ili kuipatia habari kwa wakati jamii.

Akiwasilisha mada ya wajibu wa vyombo vya habari katika uwajibikaji, Katibu Mkuu wa PPC Ali Mbarouk Omar, alisema moja ya shabaha ya jamii, ni kupata habari zenye kiwango.

 

Alieleza kuwa, habari hizo siku zote huandikwa na mwandishi pia mwenye kiwango cha ufahamu, ufuatiliaji na elimu ya kutosha juu ya jambo analoliandikia.

Katika eneo jengine, Katibu Mkuu huyo, alisema suala la utawala bora hautotimia ikiwa, hakuna uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.

Alifahamisha kuwa, uhuru wa vyombo ni sehemu kubwa ya kuiweka jamii husika kupata habari za uhakika, na kinyume chake ni kudhoofisha uhuru wa kupata habari.

“Leo tukiwa katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari, moja ya changamoto ambayo inavikumba vyombo vya habari na waandishi husika, ni mabadiliko ya kiteknologia na uchumi mdogo,’’alieleza.

Baadhi ya wadau wa habari, wamesema wakati umefika sasa kwa waandishi, kujiendeleza kielimu, ili wawe weledi wanapoandika habari zao.

Hafidh Abdi Said kutoka asasi ya KUKHAWA, alisema kada ya habari imevamiwa na waandishi wa habari husika ambao ni tegemeo la jamii, wasipojiendeleza kielimu wanaweza kuachwa nyumwa na waendesha mitandao.

 

Nae Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Chake chake Saleh Nassor Juma, alisema bado uhuru wa habari Zanzibar, umekuwa kizani, hivyo juhudi zinahitajika ili kuwaacha waandishi wa habari kutekeleza wajibu wao.

 

Hata hivyo, amesikitishwa na vyombo vinavyomilikiwa na serikali, kwa kutowapa nafasi wanapokuwa na shughuli zao, na badala yake vyombo binafsi ndio huwanavyo karibu.

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hya Mussa Said, alisema ana shaka na maslahi ya waandishi wa habari, jambo linaloendelea kuwaweka katika mazingira magumu, ya kazi zao.

Akifunga mkutano huo Kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba Tadei Mchomvu, alisema bado kisiwa cha Pemba, ni shuwari na kuwataka waandishi, kuandika habari.

Alisema, ataendelea kuwa karibu na vyombo vya habari, ili kuona wanapata habari zote zilizoko Polisi, kwani kila mmoja anamtegemea mwenzake, katika kuwahabarisha wananchi.

PPC ilishindwa kufanya shughuli ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari siku ya kawaida ya Mei 3, kutokana na Pemba kuwepo viongozi wa kitaifa .