Monday, May 20

Wananchi wanaombwa kushiriki katika zoezi la uendelezaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC George Joseph Kazi akifunguwa mkutano wa Wadau wa Uchaguzi Pemba juu ya uendelezaji wa Daftari la kudumu la wapigakuwa linalotarajiwa kuanza tarehe 2/12 mpaka tarehe 15 January 2024.
Baadhi ya Wadau wa Uchaguzi Pemba wakifuatilia kwa makini taarifa ya uendelezaji wa Daftari la kudumu la wapigakuwa linalotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao katika wilaya ya Micheweni kama ilivyotolewa na mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Thabit Idarous Faina huko katika ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi Pemba.

 

PICHA NA BAKAR MUSSA,PEMBA.

BAKAR MUSSA, PEMBA

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Zanzibar,Jaji George Joseph Kazi amewataka wananchi na Viongozi wa vyama vya Siasa Kisiwani Pemba kushirikiana na Tume hiyo katika zoezi la uendelezaji wa Daftari la kudumu la wapigakura linalotarajiwa kuanza tarehe 2/12 mpaka tarehe 15 January 2024.

Akitowa wito huo huko katika ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi Pemba wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Uchaguzi Pemba juu ya Tume hiyo kufanya zoezi hilo litakalowawezesha wapiga kura wapya kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

Alisema uendelezaji wa Daftari la kudumu la wapigakura linalotarajiwa kuanza katika wilaya ya Micheweni na kumalizika katika wilaya ya Mkoani ni kwa mujibu wa sheria za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) namba 4ya mwaka 2018.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa uandikishaji huo utawahusisha wapigakura wapya walio na sifa za kuandikishwa kuwa wapigakura kwa mujibu wa sheria za uchaguzi Zanzibar.

” Uendelezaji wa Daftari hilo utaendeshwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ikiwemo,umri, kitambulisho cha Mzanzibar, mkaazi wa kudumu wa eneo kwa muda wa miezi thalasini na sita”, alisema.

Aliwaomba wananchi wenye sifa ya kuandikishwa kwenye Daftari hilo na ambao hawajajiandikisha kujitokeza kwa wingi ili kuweza kutumia fursa hiyo muhimu ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Aidha mwenyekiti huo aliwataka wananchi na Viongozi wa vyama vya Siasa Kisiwani Pemba kuendelea kudumisha amani na Utulivu katika kipindi chote cha uendelezaji wa Daftari hilo ili zoezi liweze kwenda kama lilivyopangwa.

Alifahamisha kuwa katika zoezi hilo Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC inatarajia kuandikisha wapigakura wapya wapatao 162,606 kutokana na makadirio ya Takwimu ya Sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina alisema pamoja na hilo pia uendelezaji wa Daftari hilo utafanya shughuli nyengine ikiwemo kuhamisha taarifa za wapigakuwa kutoka eneo moja kwenda jengine la kupiga kura.

Alieleza katika zoezi hilo Tume itasahihisha taarifa za wapigakuwa, kuwasilisha maombi ya kuwafuta wapigakura waliopoteza sifa na kuwasilisha maombi ya kitambulisho kilichopotea au kuharibika, ingawaje kazi hizo hazitafanyika katika vituo vya uandikishaji bali zitafanyika katika Afisi za Tume za Wilaya.

“Tunasisitiza kuwa kila mwananchi anaeomba kuandikishwa afike katika kituo anachoomba kuandikishwa”, alisema.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa changamoto mbali mbali zinazolalamikiwa na zinaihusu Tume hiyo itazifanyia kazi ili kuona kila mwenye sifa hiyo anapata haki yake.

Nae mkuu wa kurugenzi ya huduma za sheria , Maulid Ame Mohammed akiwasilisha mada ya nafasi ya sheria ya Uchaguzi alisema kifungu cha 7(1) cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kimetowa haki kwa kila Mzanzibar alietimiza umri wa miaka 18 kupiga kura kwa uchaguzi unaofanyika Zanzibar.

Alisema kanuni za uendelezaji wa Daftari la kudumu la wapigakura za 2019 ,zinaeleza kwa undani utaratibu mzima wa uendelezaji wa Daftari la kudumu la wapigakura na kuweka fomu mbali mbali zinazotumika katika zoezi la uandikishaji na uendelezaji wa Daftari kama ziivyoelezwa katika kanuni hiyo.

“Sheria ya Uchaguzi namba 4ya mwaka 2018 kifungu cha 14(1) na 15(1)vinatambuwa aina mbali mbali za mawakala katika kazi ya uandikishaji ambao ni wakala wa chama cha Siasa na wakala wa Tume ya Uchaguzi ambae ni sheha wa Shehia husika,”alisema.

Hata hivyo mkuu wa Wilaya ya Wete Dk.Hamad Omar Bakar aliwataka Viongozi wa vyama vya Siasa kuwaasa wafuasi wao kudumisha amani na Utulivu katika kipindi chote cha uendelezaji wa Daftari hilo.

MWISHO.