Monday, May 20

Mabadiliko ya Tabianchi yatajwa kuwa chanzo cha migongano baina ya binaadamu na wanyamapori

 

NA ABDI SULEIMAN.

IMEELEZWA kuwa Mabadiliko ya Tabianchi ni moja ya chanzo cha kutokea kwa migongano baina ya binaadamu na wanyamapori, hali inayosababishwa kutokana na muingiliano mkubwa wa mahitaji na maji.

Hayo yameelezwa na Dr.Elikana Kalumanga kutoka RTI International, pia ni Meneja ushirikishwaji wa sekta binafsi katika Mardi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari za mazingira mwishoni mwa wiki Wilayani Bagamoyo.

Alisema mabadiliko yanaonekana pale mvua zinapopungua na kuwepo ukame, huku vyanzo vingi vya maji vikikauka na vilivyobakia vinatumiwa na binaadamu na wanyamapori, hali inayopelekea Wanyama kama simba kuvamia mifugo na tembo kuingia kwenye maeneo ya kilimo.

“Ukame unapokua mkubwa maeneo yanakauka ya malisho na kupelekea mifugo kuingia kwenye mashamba ya wananchi, vyanzo vya maji vilivyobakia husababisha Wanyamapori na binaadamu kugombaniana,”alisema.

Alisema mabadiliko ya tabianchi, yanachangamoto zake na madhara yake katika sekta za uhifadhi na jamii za wananchi, ukame uliokithiri na ongezeko la joto kwenye baadhi ya maeneo.

Alifahamisha kwamba ukame unapokithiri mazao hayapatikani, vyanzo vya maji maeneo mengi yanakauka na sehemu zilizobakia, zinapelekea kutokea kwa migongano baina ya wanyamapori na binaadamu kwa kugombani maji.

Dr.Kalumanga alisema mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, unaangalia namna ya kusaidia juhudi mbali mbali za serikali, katika kuziendeleza shoroba mbazo ni mapitio ya wanyamapori na shuhuli za binaadamu zinaendelea.

Alisema kwa sasa wanangalia uwezekano wa kusaidiana na serikali na wadau wengine, kuhakikisha shoroba zinahifadhiwa katika maeneo wanayopita wanyamapori, ili Wanyama wanapopata ukame katika eneo moja waweze kwenda eneo jengine kujipatia mahitaji yao bila athari zozote.

“Shorba tunazojaribu kupambana kuziokoa zinasaidia kupunguza migogoro iliyopo kati ya wanyamapori na binaadamu, kwa sababu wanyamapori wanakua na njia ya kupita kutoka eneo moja kwenda jengine hata kutoka mbuga moja kwenda mbuga nyengine,”alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuhifadhi misitu kwa kupanga miti kwa wingi, kwenye maeneo ambayo yamekua jangwa ili kurudishi upatikanaji wa hewa safi na kuondosha hewa chafu.

Hata hivyo alisema mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unatekelezwa kwenye maeneo saba, ambapo ndio maeno ya vipaombele vya serikali kama tunavofahamu serikali katika mipango yake ilianisha maeneo 61 ndio maeneo ya shoroba ya wanyamapori, na shoroba za kipaombele,

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni shoroba ya Kwakuchinja inayohusua Tarangire na Manyara, Msitu wa Amani na Nilo, Udzungwa na Hifadhi ya Nyerere, Ruaha Rungwa na Katavi, Ruaha Rungwa na Inyonga na Kigosi Moyowosi- Burigi Chaton a mahali Katavi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa JET Dr.Ellen Otaru, alisema mabadiliko ya Tabianchi yanabadilisha mfumo wa Maisha kwa binaadamu na viumbe wengine.

Alisema waandishi wa habari wananafasi kubwa kuelimisha jamii, kwa kuzuwia athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kurudisha kilichopotea kwa kupanda miti kwa wingi.

Nae Mwandishi wa habari Rahma Suleiman, alisema mazingira yanapoathirika hayamuwachi nyuma mwanamke au mtoto, wote ni wahanga wa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema kwa kiasi kikubwa sasa wanawake wameamka na kushiriki katika uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti ya matunda au biashara kwa kurudisha uoto wa asili uliopotea.

MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper/habari Portal blog
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355