Saturday, July 27

WANANCHI MJINI OLE WAISHUKURU IDARA YA KATIBA NA MSAADA WA KISHERIA ZANZIBAR

       NA ABDI SULEIMAN.

WANANCHI wa shehia ya Mjini Ole Wilaya ya Chake Chake, wamesema ujio wa wanasheria kutoka Taasisi mbli mbali Serikali, kupitia Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Pemba, umeweza kuwafumbua macho na kujua njia watakazotumia kwenda kudai haki zao kisheria.

Wamesema elimu, woga na kutokujua wapi wanapopaswa kwenda kudai haki zao ilikua ni kikwazo, hivyo ujio wa wanasheria umewajengea ujasiri wa kuanza kutia miguu katika taasisi za kisheria kuhitaji usaidia wa kupata haki zao.

Waliyaeleza hayo wakati wakizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kutolewa kwa elimu ya sheria, kwa wananchi hao ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa usimamizi wa upatikanaji wa haki kwa kesi za udhalilishaji wanawake na Watoto Zanzibar, uliofadhiliwa na UN-WOMEN kupitia European Union.

Mariyam Rashid Salumu kutoka shehia ya Mjini Ole, ameishukuru Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar kufika katika shehia hiyo, kwani mambo mbali mbali walikua wakiyaona ni kawaida tu kumbe ni udhalilishaji mkubwa waliokua wakifanyiwa.

“Sisi tunaishukuru idara hii kufika, sisi kama wanawake tulikua tunaona ni sawa kila kitu kinachotokea, tulikua tunaona tuko sahihi kumbe sivo hali ilivyo,”alisema.

Alisema ufumbuzi wamepata juu ya suala la talaka na vyeti vya vifo, kwani awali walikuwa wakikabiliwa na changamoto hizo na kuwarudisha nyuma katika harakati zao.

Nae Mariyam Salum Mussa kutoka mjini ole, alisema elimu hiyo imemsaidia kufungukua na kujua wapi ataweza kufuata haki zake kwa sasa kisheria.

“Mimi mwanamme alinitelekeza tokea ninaujauzito wa miezi minne, paka nimeweza kujifungua hadi sasa mtoto anamiaka saba, baba yake anashindwa hata kumuhudumia na mishafika katika vyombo mbali mbali vya kisheria na sijapataka haki za mwanangu,”alisema.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, alisema mradi huo ni wa   miaka mitatu na unatekelezwa katika maeneo mawili Kusuni Unguja na kusini Pemba.

Alisema wamelazimika kukutana na akinamama wanaoshuhulika na masuala ya vikoba, kwa kuwaonesha wanawake wanahaki katika masuala ya kumiliki ardhi na mali nyengine.

Alisema wananchi wataweza kujifunza mambo mbali mbali kutoka kwa watalamu wa sheria, sambamba na changamoto zilizipo wataweza kwenda kuzifanyia kazi katika taasisi zao.

Nae Mwanasheria kutoka kamisheni ya ardhi Pemba Asha Suleiman Said, alisema kwa mujibu wa sheria watu wote wanahaki ya kumiliki ardhi Mwanamke au mwanamme.

Aidha aliwataka wanaume kuwasaidia wanawake katika suala zima la mirathi baada ya mmoja ya wanafamilia kufariki, ili kuhakikisha wanawake wanapata haki zao mapema.

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka wakala wa Matukio ya Kijamii Pemba Faki Haji Faki, aliwataka wanawake kuwasajili Watoto baada ya kumzaa ndani ya siku 42, kwa ajili ya kuepukanana na faini wakati wa kuomba cheti cha kuzaliwa.

Aliwasihi akinamama kuhakikisha wanajifungulia katika hospitali na sio majumbani, kwani kufanya hivyo kunapelekea kuwa rahisi kupata kipande cha kuomba cheti cha kuzaliwa.

Hata hivyo Idara ya katiba na Msaada wakisheria Zanzibar, imemtaka mwanasheria huyo, kuhakikisha analishuhulikia tatizo la moja ya wananchi kutokupata cheti cha kuzaliwa kwa mtoto wake ambae kwa sasa anamiaka saba.

MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper/Habari portal
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355